KIUNGO wa klabu ya Juventus na timu ya Taifa ya Ufaransa, Paul Pogba, amedai kwamba kwa sasa anapiga kazi kubwa kwenye klabu hiyo tofauti na wakati anaitumikia Manchester United.
Mchezaji huyo amesema wakati yupo katika klabu ya Manchester United ilikuwa kama yupo mapumzikoni, lakini Juventus anapiga kazi kubwa.
Pogba aliwahi kuitumikia klabu ya Manchester United mwaka 2012 ambapo alipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza mara tatu kikiwa chini ya kocha Sir Alex Ferguson.
Baada ya kujiunga na klabu ya Juventus akitokea England, mchezaji huyo amekuwa na mchango mkubwa wa kuisaidia klabu hiyo kuchukua mataji mbalimbali.
“Watu wanatakiwa kujua kwamba maisha ninayoishi kwa sasa katika klabu ya Juventus ni tofauti kubwa na wakati nipo Manchester United, wakati nipo United ni sawa na kuwa likizo.
“Juventus tunajituma kwa hali ya juu na haya mataji wala hatujaiba ila tumeyapata kutokana na kujituma kwetu,” alisema Pogba.
Hata hivyo, mchezaji huyo amehusishwa na kujiunga na klabu ya Barcelona, Manchester City na Chelsea katika kipindi hiki cha usajili.