31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Pluijm presha, Omog hakuna jipya

simba-vs-yanga

Na WAANDISHI WETU,

WAKATI kocha mkuu wa timu ya Yanga, Hans Van der Pluijm, akikiri kuwa mchezo wao dhidi ya Simba ni wa presha, mpinzani wake, Joseph Omog, amesema haoni  kitu kipya  kitakachomfanya aogope na  kuwa na presha  kutoka kwa wapinzani wao Yanga,  kuelekea  katika mchezo wao utakaochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hizo zitakutana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Simba akiwa mwenyeji wa Yanga.

Pluijm ambaye ni mzoefu katika mechi hizi zenye fitina baada ya kuiongoza Yanga kwa takribani misimu mitatu,

amejipanga kupunguza presha hiyo kwa kuimarisha washambuliaji na mabeki wake, ili kuwa na kikosi bora kitakachozaa matunda Jumamosi.
Akiwa visiwani Pemba, Pluijm amekuwa na kazi ya kuhakikisha anawanoa mabeki wake kukabiliana na washambuliaji hatari wa Simba, ambao wameonekana kuwa mwiba mchungu tangu kuanza kwa ligi, washambuliaji hao ni Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib na kiungo mshambuliaji, Shiza Kichuya ambao wamekuwa wakizifumania nyavu kwenye mechi sita ilizocheza.

Akizungumza na MTANZANIA kutoka Pemba, Pluijm amesema kazi kubwa aliyoifanya kwa siku tatu mfululizo ni kuhakikisha anakipanga kikosi chake kuwa imara ili kutoka uwanjani wakiwa na matokeo mazuri.

“Ni lazima tuweke ukuta kupunguza presha hii, kwa kuzuia mashambulizi na kwa kufanya hivyo naamini tutapata matokeo mazuri, nimelazimika kufanya hivyo baada ya beki yangu kufanya vibaya kwenye mchezo uliopita dhidi ya Stand United na kujikuta tukikosa pointi tatu muhimu,” alisema.

Kocha huyo pia amefarijika zaidi na ujio wa winga wao hatari, Geofrey Mwashiuya, aliyekuwa majeruhi kwa muda sasa na tayari amejiunga na kambi hiyo.

Nahodha msaidizi wa Yanga, Vincent Bossou ambaye katika mechi dhidi ya Stand United ndiye aliyeonekana kulaumiwa zaidi amesema kamwe hawezi kurudia makosa.

“Tunajua kama mashabiki wanataka ushindi tu na ndiyo furaha yao, hivyo tutahakikisha tunazitumia vema dakika 90, yaliyopita yamepita tuangalie yajayo,” alisema Bossou.

Naye Omog alisema: “Sijaona kitu cha kunipa wasiwasi kutoka  kwa wapinzani wetu kuelekea mchezo huo kwani kikosi changu kinanifanya nijiamini zaidi.”

Hata hivyo, taarifa za uhakika kutoka kambi ya Simba zinadai kuwa Mcameroon huyo ambaye amebeba matumaini makubwa kwa wapenzi na mashabiki wa timu  hiyo, yupo katika maandalizi mazito ya kuhakikisha anaibuka na pointi tatu katika mchezo huo.

Simba inakutana na Yanga ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 16, huku Wanajangwani wakiwa nafasi ya tatu baada ya kujinyakulia pointi 10 kibindoni, wakisalia na mchezo mmoja mkononi.

Habari hii imeandikwa na Winfrida Ngonyani, Doreen Pangani na Adam Mkwepu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,625FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles