Pluijm: Nipo tayari kurejea Yanga

0
958

THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema endapo klabu itampa ofa nono, yupo tayari kurejea kukinoa kikosi hicho kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera anayetajwa kuwa mbioni kufungushwa virago.

Juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Yanga ilipokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Pyramids ya Misri, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kipigo hicho kimeonekana kuwakera Wanayanga waliokuwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi mnono ugenini kama walivyokuwa wakiaminishwa na viongozi na kocha wao huyo.

Pamoja na kuwa na nafasi ya ‘kupindua meza’ ugenini kwa kushinda dhidi ya Pyramids, watu wa Yanga wanaamini haitakuwa rahisi kutokana na kandanda iliyoonyeshwa na vijana wao nyumbani.

Hivyo basi, wanadhani Zahera uwezo wake umefikia mwisho na badala yake, lazima wapate kocha mwingine kabla hali haijakuwa mbaya zaidi.

Habari kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa tayari majina kadhaa yametajwa kuelekea kubeba mikoba ya Zahera, wengi wao wakiwa ni makocha waliowahi kuinoa Yanga kama Raoul Shungu, Ernie Brandts, Kim Poulsen na Pluijm.

Wakati MTANZANIA ikishindwa kuwapata makocha wengine hao, Pluijm amezungumza na gazeti hili juu ya tetesi hizo za kutakiwa Yanga, akisema yupo tayari kurejea Jangwani kwa mara nyingine.

Hata hivyo, alisema hadi jana hakuna kiongozi yeyote aliyefanya naye mazungumzo juu ya mpango huo.

“Hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa Yanga aliyewasiliana na mimi, kama watawasiliana na mimi, tutazungumza, tukifikia muafaka, sina tatizo,” alisema.

Pluijm aliwahi kuifundisha Yanga na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo, msimu wa mwaka 2014/15 na 2015/16.

Baadaye, nafasi yake ilichukuliwa na George Lwandamina katika mzunguko wa pili wa 2015/16, huku Mholanzi huyo akipewa Ukurugenzi wa Benchi la Ufundi.

Baada ya hapo, Pluijm alitemwa na Yanga na kutua Singida United na kuifundisha kwa msimu mmoja kabla ya kudakwa na Azam FC aliyoinoa kwa msimu moja na kutimuliwa kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here