NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van Pluijm, amesema timu yake kwa sasa haitarajii kushuka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo ni muhimu kwao kushinda kila mechi.
Yanga juzi ilipanda kileleni kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 36 baada ya kuifunga Ndanda FC bao 1-0, lililofungwa na Kelvin Yondani kwa mkwaju wa penalti, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Pluijm alisema timu nzuri ni ile inayocheza mpira mzuri na hatimaye kupata matokeo mazuri, hicho ndicho wanachokifanya wachezaji wake.
“Ninachowaelekeza ndicho wanachofanya, ingawa kuna wakati walikuwa wanakaa na mpira, kitu ambacho sikifurahii, napenda wawe haraka na kutoa pasi ndefu,” alisema.
Alisema, hata hivyo timu yake iliweza kutengeneza nafasi nyingi za kupachika mabao, licha ya tatizo la umaliziaji lililoonekana kuwasumbua.
Alieleza, kwa ujumla mchezo ulikuwa mzuri, kwani Ndanda ni timu nzuri, ambapo awali walitoka nayo sare ya bao 1-1 na sasa wamewafunga.