KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, amesema watatimiza mipango ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kushinda mechi zote 21 zilizobaki, sawa na pointi 63.
Yanga, yenye pointi 23 katika nafasi ya pili, imeshushwa kileleni na Azam FC iliyofikisha pointi 25 kwenye msimamo wa ligi, huku timu zote zikiwa hazijapoteza mchezo wowote hadi sasa katika mechi tisa walizocheza.
Kwa sasa ligi imesimama kupisha usajili wa dirisha dogo utakaofunguliwa Novemba 15, mwaka huu pamoja na mechi za timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Kombe la Chalenji, hivyo itaendelea tena Desemba 12, mwaka huu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Pluijm alisema anafurahishwa na mwenendo wa kikosi chake hadi sasa, huku akieleza kuwa mikakati waliyojiwekea ligi itakapoendelea ni kuhakikisha wanashinda mechi zilizobakia.
“Hatutaki kubakisha pointi yoyote uwanjani kwenye mechi zetu zinazokuja, upinzani ni mkubwa sana, hivyo tutajipanga kushinda mechi zote,” alisema.
Kama hesabu za Mholanzi huyo zitakaa sawa na Yanga ikatetea ubingwa wake bila kufungwa mchezo wowote, itakuwa imefikia rekodi za Azam iliyochukua ubingwa bila kupoteza msimu wa 2013/14 na Simba msimu wa 2009/10.
Akizungumzia changamoto za michuano ya Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, Pluijm alisema anajua namna ya kupambana na wingi wa mashindano hayo ndani ya muda mfupi, huku akidai hataweka wazi usajili wake wa dirisha dogo.
“Siwezi nikaongelea nitasajili mchezaji wa namna gani au wa nafasi ipi kwa sasa, nitafanya hivyo pale tu taratibu za kumsajili mchezaji ninayemtaka zitakapokamilika,” alisema.