NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans Van der Pluijm, ameutunishia misuli uongozi wa klabu hiyo, akipinga kuweka kambi mjini Bagamoyo ili kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Agosti 22 mwaka huu, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo juzi iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City, katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Sokoine mkoani humo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, zililipasha MTANZANIA jana kuwa mikakati iliyopo ni kuipeleka kambini moja kwa moja timu hiyo ambayo inarejea leo kutoka jijini Mbeya, ili kujiandaa na mchezo huo.
Chanzo cha habari hizi kilisema uongozi umefikiria kikosi kiingie kambini kwa siku tatu mjini Bagamoyo na kurejea jijini Dar es Salaam siku ya mchezo.
“Uongozi umedhamiria timu itakaporudi moja kwa moja ielekee Bagamoyo, lakini kocha anaonekana kupinga kwa madai ya kuwa kufanya hivyo kutawavuruga wachezaji.
“Kocha anaamini kambi ya wiki mbili waliyoweka Mbeya inatosha, hivyo hata wakirejea kambi iwekwe hapa hapa na siyo nje ya mji,” alisema.
Timu hiyo ambayo ilikuwa kambi mjini Mbeya, tayari imecheza mechi tatu za kirafiki mkoani humo kujitayarisha na mchezo wake dhidi ya Azam.