WAKATI baadhi ya mashabiki wa Yanga wakianza kuponda uwezo na ubora wa straika mpya wa klabu hiyo aliyesajiliwa kwa fedha nyingi, Mzambia Obrey Chirwa, kocha Hans van der Pluijm, ameamua kumkingia kifua.
Chirwa ambaye ametua Yanga kwa kitita cha zaidi ya shilingi milioni 200 akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, ameshindwa kuonyesha makeke yake kwenye mechi tatu za kimataifa alizocheza hadi sasa tangu asajiliwe na miamba hiyo ya Jangwnai.
Lakini, Pluijm aliliambia MTANZANIA jana kuwa hawezi kumhukumu mchezaji huyo kwa michezo michache aliyocheza hadi sasa.
“Makelele ya mashabiki hayawezi kunifanya nishindwe kumwamini Chirwa kwani michezo aliyocheza haitoshi kutathmini na kupata jibu la uwezo wake.
“Ni mshambuliaji mwenye kiwango kizuri, ninamwamini na nitampa muda wa kujiweka vizuri hadi pale kiwango chake kitakapokaa sawa,” alisema Pluijm.
Pia kocha huyo alisema kwamba kwa sasa hana mpango wa kusajili mchezaji mwingine katika kikosi chake akiamini kwamba kitakuwa bora zaidi mara tu atakapokifanyia maboresho.
“Najua kuna malalamiko kuhusu wachezaji lakini sina mpango wa kuongeza wala kupunguza mchezaji kwa sasa,” alihitimisha Pluijm.