22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm ambakisha Msuva Yanga

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van Pluijm, amembakisha winga Simon Msuva kwenye timu hiyo kwa mwaka mmoja zaidi, ili kumtengeneza vyema kabla ya kutimkia Afrika Kusini.
Wiki iliyopita Msuva alikwenda kufanya majaribio katika timu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini, ambapo baada ya kurejea nchini ilielezwa amefaulu majaribio hayo.
Pluijm, aliyeongozana na Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, walifanya ziara maalumu kwenye Ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Limited jana, inayochapisha gazeti hili, Dimba, Bingwa, Rai na The African.
Pluijm alisema Msuva anatakiwa kusubiri kwa mwaka mmoja kabla ya kwenda huko, ambapo amepanga kumwongezea mbinu zaidi na uwezo.
“Alikwenda kwenye majaribio katika kipindi ambacho sikutarajia, lakini nilikuwa nimemshauri abakie hapa kwa mwaka mmoja ili nimuongezee mbinu na uwezo zaidi kwa ajili kufanya vizuri huko,” alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea, Medeama na Ashanti Gold zote za Ghana, pia alimtakia kila kheri Mrisho Ngassa, aliyesajiliwa na timu ya Free States Stars ya Afrika Kusini na amemtaka abadilishe mtazamo wake.
“Ngassa anatakiwa kubadilisha mtazamo wa uchezaji wake, hiyo haitoshi, anatakiwa pia azingatie na kufikiria soka na hii ni pale anapokuwa na mpira na nyendo zake akiwa hana mpira.
“Namjua Ngassa ni mchezaji mzuri sana aliyebarikiwa kipaji nchini, lakini hatakiwi kuishia kushambulia tu, anatakiwa pia kurudi nyuma kukaba pale timu inapokuwa haina mpira, si unamuona Ronaldo (Cristiano), mbali na kushambulia kuna muda unamuona anarudi nyuma kusaidia timu kukaba, je, hilo unaliona kwa Ngassa,” alihoji Pluijm.
Mholanzi huyo aliyeondoka nchini jana usiku kuelekea nchini Ghana kwa mapumziko, alisema Ngassa akifanya hayo atafanikiwa na kufika Ulaya, kuhusu kuziba pengo lake Pluijm amedai hivi sasa anatafuta mchezaji wa kiwango cha juu kuliziba.
Timu ya Yanga kwa sasa ipo mapumzikoni hadi Mei 30, mwaka huu, itakapokusanyika tena kwa ajili ya kuanza maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame, itakayofanyika nchini kuanzia Julai 11 hadi Agosti 2, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles