Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KATIKA kukabiliana na changamoto ya mafuriko ambayo imekuwa ikiwasababishia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam usumbufu mkubwa, kampuni ya Plasco Limited imesema imekuja na teknolojia mpya iliyowezesha upatikanaji wa mabomba yatakayosaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Alimiya Osman, alisema jana kuwa teknolojia hiyo imewezesha uzalishaji wa mabomba imara ya Weholite, ambayo ni mepesi, yenye kipenyo kikubwa, yaliyotengenezwa na malighafi zenye ubora za polyethilini (high density polyethylene – HDPE).
Alisema mabomba hayo yanafaa kutumika wakati maji yanakuwa na msukumo mdogo kwenye ujenzi wa miundombinu ya mifumo ya maji taka, mifumo ya utakatishaji wa maji taka, kutengeneza makaravati, mabomba ya kupeleka na kupitisha maji baharini na usambazaji wa maji katika miradi ya umwagiliaji.
“Matumizi yote haya yanafanya mabomba ya Weholite kufaa kutumika sio kwenye miradi ya manispaa bali pia kwamatumiziyaviwandani.
“Plasco ndio kampuni pekeeyenye leseni ya kutengeneza mabomba yanayotumia teknolojia ya Weholite nchini Tanzania, yametengenezwa kwa malighafi bora za polyethilini (HDPE), ambayo ni ya kipekee kwa ubora mkubwa kiasi cha kuweza kuhimili changamoto ya mafuriko katika maeneo ya mijini.
“Weholite ni imara na inadumu kwa kipindi kirefu na inawezesha upitishaji mzuri wa maji kwa zaidi ya asilimia 30. Inapatikana kwa ukubwa hadi kipenyo cha ndani cha 2200mm ambayo inafanya kuwa bora kwa kupitisha maji kutoka maeneo yenye tatizo la mafuriko na hivyo kuwa msaada kwa wakazi wenye changamoto hiyo,” alisema Osman.
Mtaalam huyo alibainisha sifa zingine za kipekee za Weholite kuwa inarahisisha kazi za uhandisi wa masuala ya maji zaidi ya mabomba ya zege, ambayo hudumu kwa kipindi kirefu, sifa ambazo zinayafanya kuwa suluhisho pekee kwa upitishaji wa maji mengi.
Alisema hali ya sasa miundo mbinu ya maji katika sehemu nyingi imechakaa na haina uwezo wa kuhimili kupitisha maji mengi kwa wakati mmoja, lakini kwa teknolojia ya Weholite tunaweza kubuni mifumo ambayo itatoa suluhisho kwa miaka 100 ijayo.
Osman alieleza kuwa Plasco Ltd imekuwa ikifanya kazi na manispaa za Tanzania na sekta binafsi kupitia makampuni ujenzi yanayojenga miradi mbalimbali kwa kutumia mabomba ya Weholite.
Moja ya mradi mkubwa ambao mabomba haya yametumika katika mifumo ya kusafirisha maji ni uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Terminal III Dar es Salaam, kulingana na Wahandisi wa mkandarasi mkuu wa mradi huo, BAM International alisema “Teknolojia ya Weholite iliwezesha ujenzi wa mifumo ya kusafirisha maji kuwa wa haraka na gharama nafuu japo ulifanyika wakati wa msimu wa mvua”.
Alisema mifumo ya Weholite ni suluhisho jipya la ubunifu wa bomba ambalo linaweza kuleta thamani kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, kwani yanatengenezwa nchini kwa kutumia teknolojia za viwango vya kimataifa ambazo zimekuwa zikitumika katika nchi za Afrika Kusini, Ulaya, Amerika Kaskazini na sasa inapatikana nchini Tanzania.
Alieleza kuwa kwa Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi zaidi ya milioni tano ambalo limekuwa hatarishi kutokana na changamoto hata ikinyesha mvua kwa muda mfupi maeneo yake mengi yamekuwa yakijaa maji na barabara nyingi kupitika kwa shida kutokana na kujaa madimbwi ya maji kutokana na kuchakaa kwa miundombinu ambayo haina tena uwezo wa kuhimili kasi ya ukuaji wa mji na ongezeko kubwa la watu, suala hilo linatakiwa kutafutiwa ufumbuzi.
Alisema tatizo lililopo kwa sasa ni kwamba mifumo inazidiwa pia kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambapo kunanyesha mvua kubwa katika vipindi tofauti na ongezeko la makazi mapya, wakati hakuna mifereji ya kutiririsha maji ya mvua, suala ambalo linaweza kutatuliwa kwa matumizi ya mabomba hayo..
“Mafuriko ya Dar es Salaam yanaendelea kuathiri shughuli za kiuchumi za jiji wakati wa kila msimu wa mvua. Kulingana na utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia, jiji lilipata hasara ya asilimia mbili ya Pato la Taifa (GDP) kwa sababu ya mafuriko mijini mnamo 2018.
“Wataalam wanasisitiza kwamba kuwa na miundombinu bora, mipango, kutumia vifaa bora vya mifereji ya maji kama vile Mabomba ya Weholite, changamoto hii inaweza kuepukwa na kuwezesha hali ya maisha ya wananchi kuwa bora hadi kwa vizazi vijavyo,” alisema..