NICE, UFARANCA
BEKI wa kati wa timu ya Taifa ya Hispania, Gerard Pique, ameweka wazi kwamba timu hiyo haikuwa na ubora wa kutosha kuweza kutetea ubingwa wa Euro 2016 msimu huu.
Timu hiyo ilichezea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Italia na kutolewa katika michuano hiyo nchini Ufaransa, hivyo Pique amedai kwamba hawakuwa bora kuweza kutetea ubingwa huo.
Italia imeonesha kwamba ilikuwa na lengo la kutaka kulipa kisasi cha mwaka 2012 ambapo walipokea kichapo cha mabao 4-0 katika michuano hiyo hatua ya fainali dhidi ya Hispania.
“Nadhani hatukustahili kusonga mbele katika michuano hii kutokana na ubora wa kikosi chetu, lakini tulikuwa na lengo la kutaka kusonga mbele ila ushindani ulikuwa mkubwa na wenzetu walikuwa bora zaidi.
“Baada ya kupoteza mchezo wetu wa awali dhidi ya Croatia nilisema kwamba tutakuwa na wakati mgumu wa kuweza kuendelea, niliona kuwa ubora wetu umekuwa wa chini sana na nilijua kwamba hatuwezi kufika kokote.
“Kikosi chetu kina wachezaji wazuri lakini si wa kutetea ubingwa, ila ninaamini katika michuano mingine tutaweza kufanya vizuri kutokana na maandalizi ambayo tutayafanya,” alisema Pique.