29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda ashauri mfumo bora mikopo ya halmashauri

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ameshauri Serikali kuja na mfumo bora wa utoaji mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ili kuyasaidia makundi yaliyokusudiwa.

Aprili 13, mwaka huu Serikali iliziagiza halmashauri zote nchini kusitisha utoaji mikopo hiyo hadi utaratibu mwingine utakapoelekezwa.

Washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali kutoka katika Kata ya Pugu, Dar es Salaam.

Akizungumza Julai 6,2023 wakati wa kufunga mafunzo ya wajasiriamali katika Kata ya Pugu, amesema kunatakiwa kuwepo kwa mfumo mzuri wa kubainisha makundi ya wahitaji wa mikopo hiyo.

Mafunzo hayo yaliyoshirikisha wanawake kutoka maeneo mbalimbali ya Pugu yaliandaliwa na Diwani wa Kata hiyo Imelda Samjela, kwa lengo la kuwajengea uwezo waweze kunufaika kiuchumi.

“Tunahitaji uwepo mfumo mzuri wa mikopo ya asilimia 10 kwa kubainisha makundi ya wahitaji, viongozi wetu waone namna bora ya kuboresha.

“Acheni vikundi viwe vya hiyari watu wanaojuana na kuaminiana, utakapoanza kuvipanga unaweza kuleta mgogoro,” amesema Pinda.

Pinda amempomgeza diwani huyo kwa kuandaa mafunzo hayo na kushauri washiriki wapatikane kuanzia ngazi ya mashina kwa sababu huko ndiko chama kinapoanzia.

“Ukitaka kwenda katika mstari ulio sahihi ukikosa mafunzo, unakokwenda utakuwa unabahatisha. Wajumbe wa shina ni viongozi muhimu, muende kila tawi mpate washiriki,” amesema.

Naye Diwani wa kata hiyo, Samjela amesema mafunzo hayo ya siku tatu yamelenga kuwaongezea uwezo wanawake waweze kujikwamua kiuchumi na kuahidi kuandaa mengine.

Kwa mujibu wa diwani huyo wanawake hao wamefundishwa kutengeneza vitu mbalimbali kama vile batiki, sabuni, dawa za usafi, mafuta ya kupakaa na jinsi ya kujisajili Brela.

Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi amesema umefikia asilimia 90 na kwamba wamejenga pia shule mpya ya msingi ya Mizengo Pinda.

Hata hivyo diwani huyo amesema kero kubwa kwa sasa ni kukosekana kwa daraja katika eneo la Kinyamwezi na dampo la Pugu Kinyamwezi ambalo linalalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles