24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda afunguka urais 2015

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Fredy Azzah, Dar

BAADA ya jina lake kutajwa kuwa miongoni mwa watu watakaowania urais, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema zipo taratibu ndani ya chama chake za kutangaza kuwania nafasi hiyo na kusema kinachoendelea hivi sasa ni juhudi binafsi za watu.

Pinda alisema hayo jana nyumbani kwake jijini Dar es Salaam alipokutana na wahariri wa gazeti hili, kuzungumzia masuala mbalimbali yanayolikabili taifa.

Hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti taarifa za Pinda kukutana na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza akidaiwa kuwaeleza nia yake ya kuwania nafasi hiyo ya juu nchini.

“Nadhani lengo lilikuwa tu kufanya huyu mtu naye aonekane kwa chama kavunja taratibu.

“Kama ni kweli yaliyosemwa, chama kitachukua taarifa, tutakwenda na sisi kujieleza, kwani kuna tatizo gani?

“Zipo taratibu ndani ya chama, kitendo chochote unachofanya ambacho kinavunja sheria za chama chako, zipo taratibu zake, suala la taribu ni muhimu, bado tuheshimu taratibu” alisema Pinda.

Kwa mujibu wa Pinda, taarifa za yeye kutaka kugombea urais aliziona katika vyombo vya habari na kusisitiza taarifa hizo zilisababisha watu kutoka sehemu mbalimbali ya nchi kuulizia.

Aidha waziri mkuu alitaka kuanzia sasa watu kujadili mambo ya msingi yatakayowezesha kupatikana kwa rais anayefaa wa 2015.

“Lakini kikubwa tukipersonalize sana si vyema ila tuzungumze mambao ya msingi tunayotaka mtu awe nayo na sifa tunazotaka mtu huyo awe nazo, nachelea tunapoteza muda mwingi kujadili watu.

“Wanaweza kujitokeza hata watu 100, lakini kati yao anaweza asiwepo hata mmoja, wananchi ndiyo wanaojua ni nani atakuwa rais, ziko taratibu ndani ya chama za namna ya kutoa habari kama hizi, kwa sasa hivi chochote utakachosema kitaleta shida, hata kama uki-personalize ukamwita mtu this is between you and me (hili ni kati yangu mimi na wewe), na yeye atatoka na kwenda kumwambia mwingine halafu aseme nimeambiwa hili ni kati yangu mimi na wewe,” alisema.

Pinda alisisitiza kuwa jambo la urais ni kubwa hivyo ni vyema watu wakaaswa kufuata taratibu za chama.

“Hii ya chini chini ni juhudi za watu binafsi tu,” alisema Pinda.

Alipoulizwa kama anazo ndoto za kuwania nafasi hiyo, Pinda alisema “For the appropriate (kwa muda mwafaka), wala sintosubiri ndoto itimie, nitafuata taratibu, nitaitisha press conference (mkutano na waandishi wa habari) niseme,” alisema.

Alisema kuwa, kwenye jamii mjadala uliopo wa kumjadili Pinda kwa sifa zake na vitu alivyofanya ni jambo lililo jema hata kama hajaonyesha nia yoyote.

“Hata mjadala uliopo magazetini ni mzuri tu, kikubwa tujue tu tuki-personalize we miss the boat.

Bila kujali ni nani, tuone ni nini anacho cha kutufikisha kule tuendako, nachelea sana ninapoona watu wanapoteza muda mwingi kunijadili mimi na mtu mwingine, kuna kundi huko (wananchi) ndio watakaoona ni nani ndiye anafaa,” alisema.

Apata hofu na wanaounga mkono wagombea

Kuhusu makundi ya watu wanaojitokeza na kuunga mkono wagombea, Pinda alisema “Tatizo jingine ninaloliona, ni watu kuniona nafaa wakitegemea nitawapa kitu fulani, mtu corrupt (mla ruswa) anakuja leo na kuniambia nafaa ili baadaye nije kulipa fadhila.

Wanakuja wanakusonga mpaka unakuwa unashindwa kufanya maamuzi binafsi, inatakiwa unakuwa huru hata ukija kufanya maamuzi kama ni ya kumteuwa mtu wa kukusaidia umteue hata yule ambaye hakusogelea kabisa kwenye kampeni zako, si kukaa na kusikiliza hawa wanaokuvisha vilemba vya ukoka” alisema.

Uimara wa chama

Alisema kuwa, pamoja na kujitokeza kwa makundi mengi ya urais, bado chama hicho kipo imara na kina nafasi ya kuyaweka sawa.

“Mnapofika kwenye vipindi vya chaguzi mengi yanajitokeza, kushutumiana na mambo kama hayo, lakini nafasi bado ipo ya kuwaita na kuwaonya.

Wote waliojitokeza wajue kuwa wao ni watoto wa baba mmoja, wasilumbane waendeshe kampeni za staa, inatakiwa tukifika mwisho, yeyote atakayepata iwe rahisi kusema nakaa naye tupeleke mambo mbele,” alisema.

Katiba

Kuhusu suala la katiba, alisema kinachoendelea bungeni kwa sasa ni matokeo ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuwa, hata kwenye kamati kulikuwa na changamoto nyingi na wakati mwingine ilibidi wakubaliane kutokubaliana.

“Mimi nipo kamati namba moja, na kule yuko Kessy (Ally Kessy, Mbunge wa Nkasi) na Lembeli, (James Lembeli Mbunge wa Kahama), mtaweza kuona kazi iliyokuwapo, Wakati mwingine ilibidi tukubaliane kutokubaliana,” alisema.

Alisema kuwa, mchakato huo ulipofikia sasa baadhi ya wananchi wanaona misimamo ya kisiasa ikiwa ni ule wa  Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wa kutaka serikali tatu na ule wa CCM wa serikali mbili ndio uliosababisha yote yanayoendelea.

“Ni kweli suala la Serikali mbili sisi ndio tulikuja nalo na la Serikali tatu tunasema kama kweli haya ni mawazo ya wananchi mbona takwimu za tume ukiangalia hazisemi hivyo.

“Ukiniuliza mimi binafsi nitakwambia mtindo wa serikali mbili tulionao naupenda zaidi, muungano huu tulionao ukisema tuende kwenye wa aina nyingine hapo ni kila mtu na lwake,” alisema Pinda.

Alisema kuwa, watu waliozaliwa kabla ya mwaka 1964 ni wachache kulinganisha na wale waliozaliwa baada ya mwaka huo.

“Kabla ya mwaka 1964, tulikuwa tumetoka kwenye ukoloni na muda mfupi wa uhuru, ukiuliza waswahili wa bara kwa nini mnataka serikali tatu kila mtu atakwambia lake,” alisema.

Alisema kuwa, kiusalama muundo wa sasa wa muungano ni bora zaidi ya mwingine wowote.

Alisema pia kuwa, ni vyema watu wakajiuliza kama kulichanganya suala la muundo wa katiba kwenye mambo yote yaliyotafutiwa maoni ni sahihi ma ingetakiwa kuwe na njia nyine ya kuwahoji wananchi.

Hata hivyo alisema kuwa, kwa wakati huu ni muhimu sana kama  Katiba Mpya ipatikane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles