27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

PIKIPIKI ZILIVYOONGEZA UFAULU DODOMA, KIGOMA

Na LILIAN LUNDO – MAELEZO

MRATIBU Elimu Kata (MEK) ni mmoja kati ya kiungo kikubwa kati ya ofisi ya elimu ya wilaya na shule za Serikali katika ngazi ya kata ambaye ndiye mfuatiliaji mkubwa wa maendeleo ya elimu ndani ya kata.

Shughuli nyingine zinazofanywa na MEK ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya taalamu ya wanafunzi katika kata yake, kukagua ufundishaji wa walimu, kufuatilia mahudhurio ya wanafunzi pamoja na kusimamia vikao mbalimbali vya shule zilizoko katika kata yake.

Asilimia kubwa ya waratibu elimu kata walikuwa wanashindwa kufikia malengo ya kazi zao kutokana na changamoto ya usafiri, ambapo wengi wao walikuwa wakitumia usafiri wa baiskeli ambao haukuwa rafiki kutokana na kazi yao ya kukagua shule zote katika kata wanazozisimamia.

Serikali kwa kuliona hilo, kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania     (EQUIP-T)  ilitoa pikipiki kwa kila MEK katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Lindi, Shinyanga, Simiyu na Mara ili kurahisha ufuatiliaji wa mendeleo ya shule zao kwa urahisi.

Pikipiki hizo zimeleta mafanikio kwa kupunguza idadi ya wanafunzi watoro, kiwango cha ufaulu kupanda kutokana na ukaguzi wa mara kwa mara wa walimu pamoja na matatizo kutatuliwa kwa haraka kufuatia taarifa za shule kufika ofisi za wilaya kwa wakati.

Sweetbert Malimi ni Mratibu Elimu Kata wa Sanzawa Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma anasema pikipiki imemuwezesha kushughulikia kwa wakati matatizo yanayotokea katika shule anazozisimamia tofauti na kipindi ambacho hakuwa nayo.

Anaendelea kusema kuwa matatizo yalipokuwa yakitokea katika shule anazosimamia yalikuwa yakimsubiri MEK hata kwa mwezi mzima. Lakini sasa hivi hali imekuwa tofauti kutokana na urahisi wa kufikika kuzitembelea shule zake hata mara mbili kwa wiki.

Mratibu Malimi anasema kuwa ameweza kukagua na kufuatilia kwa wakati maendeleo ya taaluma ya wanafunzi pamoja na ufundishaji wa walimu ambapo kabla ya kuwa na pikipiki, baadhi ya walimu walijisahau kutokana na kutokaguliwa mara kwa mara.

Anasema ufuatiliaji huo umeletea mafanikio makubwa katika Mkoa wa Dodoma, ambapo ufaulu wa darasa la saba kwa Wilaya ya Chemba peke yake ulipanda kutoka asilimia 30 mwaka 2015 mpaka asilimia 46 mwaka 2016. 

Kwa upande wake Mratibu Elimu Kata wa Songambele iliyoko Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, anasema kuwa katika kata yake ana shule sita za kuzifuatilia ambapo kabla ya kupata pikipiki alikuwa akitumia baiskeli kutembelea shule hizo na aliweza kuzitembelea mara moja kwa wiki.

Baada ya kupata pikipiki anaouwezo wa kutembelea shule hizo mara tatu hadi nne kwa wiki akifuatilia maandalio ya walimu, maazimio ya kazi, utengenezaji wa zana za kujifunzia na kufundishia, mahudhurio ya wanafunzi pamoja na kuhudhuria vikao vya kamati ya shule.

Aidha, anasema kuwa kutokana na ufuatiliaji huo wa mara kwa mara katika shule hizo kumesaidia kuwapo kwa umakini mkubwa wa ufundishaji wa walimu kwa kufuata taratibu za ufundishaji kama vile kuwa na maandalio, maazimio ya kazi pamoja na kuwa na zana za ufundishaji.

Pia anasema kuwa kwa kutumia pikipiki aliyopewa amekuwa akiwatembelea wazazi ambao watoto wao ni watoro, na kuwashauri juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wao na wazazi wenyewe. Juhudi hizo zimesaidia wazazi wengi kubadilika na wamekuwa na mtazamo chanya kwa kushirikiana na walimu katika kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya taaluma ya watoto wao.

Naye Mratibu Elimu Kata wa Kagera, Manispaa ya Kigoma mkoani Kigoma,  Jovitus Augustus anasisitiza kuwa kabla ya kupewa pikipiki kata yake ilikuwa na changamoto ya utoro kwa wanafunzi pamoja na ufaulu duni wa wanafunzi wa darasa la saba.

“Pikipiki niliyopewa kupitia mpango wa EQUIP-T umeniwezesha kutengeneza mipango kazi ya wiki na kuisambaza katika shule zote za kata pamoja na kufuatilia utekelezaji wake,” anafafanua Jovitus.

Anasema pikipiki hiyo imemuwezesha kukagua utekelezaji na utoaji taaluma kwa kukagua maazimio ya kazi na maandilio ya somo pamoja na kufanya vikao vya mara kwa mara na walimu ili kupata maelezo ya walimu walioshindwa kutekeleza wajibu wao.

Aidha, kupitia juhudi hizo zilizofanyika, ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba shule za msingi za Kagera na Mgumile ulipanda pamoja na  mahudhurio ya walimu na wanafunzi katika kata hiyo umeongezeka.

Pia umeanzishwa utaratibu wa mitihani ya kata kwa darasa la saba pamoja na kuweka kambi kwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani wa darasa la saba.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazoezi Bunda iliyoko Halmashauri ya Mji wa Bunda, mkoani Mara, Mwalimu Vicent Ndunguru anaipongeza Serikali kupitia Mpango wa EQUIP-T kwa kutoa pikipiki kwa waratibu elimu kata ambao kwa kiasi kikubwa umewarahisishia utendaji kazi wao.

Anasema kuwa mambo mengi yalikuwa hayaendi yalivyotakiwa kuwa kutokana na MEK kutotembelea shule mara kwa mara kwa sababu ya kukosa usafiri wa uhakika.

Kupatiwa pikipiki MEK imekuwa chachu ya kutembelea shule zilizochini ya kata yake mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya shule na kuwasilisha taarifa zake ofisi za elimu wilaya kwa wilaya na kwa wakati.

Mwalimu Ndunguru ambaye pia ni Msaidizi wa MEK katika kata ya Nyasura anasema MEK huyo amekuwa msimamizi bora wa elimu kwa kuitisha vikao vya mara kwa mara kujadili maendeleo ya shule katika kata yake, shule ya Msingi Mazoezi Bunda ndio eneo lilochaguliwa kwa ajili ya kufanyia mikutano hiyo.

Ndunguru anasema MEK huyo amekuwa chachu ya maendeleo ya shule zilizoko katika kata hiyo hasa baada ya kuwa na uhakika wa usafiri ambao kwa asilimia kubwa umemuwezesha kufanya kazi zake kwa urahisi na hata kufikia malengo aliyowekewa na mwajiri wake na yale aliyojiwekea yeye mwenyewe katika kuhakikisha ubora wa elimu unaoongezeka siku hadi siku kutoka ngazi ya kata mpaka Taifa.

Mwalimu Ndunguru ameishukuru Serikali kwa jitihada zake katika kujali sekta ya elimu na kuiomba Serikali kuendeleza utaratibu wa ugawaji wa pikipiki kwa waratibu elimu kata wa mikoa mingine iliyobaki ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi kama ambavyo wenzao waliopewa pikipiki walivyoweza kufanikiwa kupandisha kiwango cha ufaulu na kukomesha tatizo la utoro kwa wanafunzi.

Serikali kupitia mpango huo pia umetoa vishikwambi kwa waratibu elimu kata hao, ambao wamekuwa wakitumia vifaa hivyo kwa ajili ya kupokea taarifa kutoka kwa walimu wakuu wa shule wanazozisimamia na wao kuzituma taarifa hizo ofisi za elimu za wilaya.

Mpango wa EQUIP-T tayari umeshatoa jumla ya pikipiki 1,000 kwa waratibu elimu kata wa mikoa ya Dodoma, Kigoma, Lindi, Shinyanga, Simiyu, Shinyanga na Mara ambazo zilitolewa kati ya mwaka 2014 na 2015 na wanawawezesha waratibu hao kupata fedha ya mafuta na utengenezaji wa pikipiki hizo kila mwezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles