MSHAMBULIAJI wa timu ya Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang, ameipa pigo kubwa klabu ya Arsenal baada ya kuthibitisha kwamba hana mpango wa kujiunga na klabu hiyo.
Arsenal ilikuwa moja kati ya klabu kubwa kutoka Ulaya iliyokuwa ikitaka kumsajili mchezaji huyo raia wa Gabon ambaye ametajwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika.
Kocha wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger, alitajwa kuwa kati ya wanaotamani kupata saini ya mchezaji huyo ambaye amekuwa katika kiwango bora katika michuano ya Bundesliga msimu huu.
Arsenal walitajwa kuwa katika mbio hizo wakiwa na takribani pauni milioni 44 ili kufanikisha dili hilo na klabu ya Dortmund.
Aubameyang amefanikiwa kufunga mabao 24 katika michezo 23 kwenye mashindano yote aliyoshiriki msimu huu na kufanya kuzivutia timu kubwa Ulaya.