28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

PETER TINO: ALIIPELEKA STARS LAGOS 1980

Na HENRY PAUL-DAR ES SALAAM


UNAPOZUNGUMZIA historia ya soka nchini Tanzania si rahisi kuacha kulitaja jina la Augustino Peter maarufu Peter Tino, kwa sababu yeye ndiye aliyeipeleka timu ya taifa, Taifa Stars katika michuano ya fainali ya Kombe la Mataifa Huru Afrika mwaka 1980.

Tino mbali na kumudu kucheza vyema nafasi ya ushambuliaji wa kati sentafowadi, pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji ikiwa ni pamoja na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga chenga za maudhi, mashuti makali na ilikuwa si rahisi kukosa kufunga bao akibaki yeye na kipa.

Hivi karibuni SPOTI KIKI lilimtafuta mkongwe huyo ambaye hivi sasa amegeukia kazi ya ujasiriamali na kufanya naye mahojiano kuhusiana na kitu gani ambacho hawezi kukisahau zaidi wakati anacheza soka ya ushindani miaka ya nyuma.

Katika mahojiano hayo, Tino anazungumzia kitendo cha kuipeleka timu ya taifa, Taifa Stars katika michuano ya fainali ya mataifa huru Afrika yaliyofanyika mjini Lagos, Nigeria mwaka 1980.

“Nakumbuka mechi niliyoipeleka Taifa Stars kucheza fainali ya Mataifa Afrika, ulikuwa ni mchezo wa awali wa kufuzu michuano hiyo ambapo niliisawazishia timu yangu bao 1-1 katika dakika ya 88, mchezo uliochezwa katika Mji wa Ndola nje kidogo ya Lusaka, Zambia Agosti   26, 1979.

“Taifa Stars tulipata tiketi hiyo kutokana na faida ya bao la ugenini kwani katika mechi ya kwanza tuliyocheza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru) tuliwafunga timu ya Taifa ya Zambia (KK 11) bao 1-0.

“Nakumbuka bao la kusawazisha lilitokana baada ya Zambia kupata mpira wa kona na hivyo wachezaji wote walikwenda golini kwetu kutaka kufunga kona hiyo na kuacha mabeki wawili tu ambao walikuwa wananilinda mimi.

“Baada ya kona kupigwa kipa wetu Pondamali alipiga ngumi mpira ule na kumfikia kiungo Hussein Ngulungu ambaye naye baada ya kuumiliki alipiga pasi ndefu kwangu ambapo wakati huo nilikuwa nimebaki na mabeki wawili tu.

“Nilipokuwa nakokota mpira mabeki hao wawili wakawa wanarudi nyuma na ndipo nilipompiga chenga beki mmoja na kubaki na mmoja ambaye nilimzidi mbio na nilipofika kama mita 18 toka golini niliachia shuti kali lililomshinda kipa Efford Chabala na mpira kutinga wavuni.

“Baada ya kusawazisha bao hilo uwanja mzima ulinyamaza na kuwa kimya kabisa isipokuwa kwa Watanzania wachache waliokuwepo uwanjani hapo ambao walikuwa wanashangilia.

“Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika matokeo yalikuwa ni sare ya bao 1-1, lakini kwa sare ile Stars tulipata tiketi ya kwenda kucheza kwa mara ya kwanza na ya mwisho fainali za Mataifa Afrika Lagos, Nigeria 1980.

“Nakumbuka katika mechi ile Wazambia wakiongozwa na Rais wao wa wakati huo, Kenneth Kaunda, walishangilia kwa nguvu kwa muda wa dakika 88 na sisi baada ya kusawazisha bao lile tuliwanyamazisha kwa dakika mbili tu.

Akizungumzia kujituma kwa wachezaji wa sasa wakiwa uwanjani kulinganisha na wa zamani wakati yeye anacheza soka, Tino anazungumzia kwa kifupi akisema:

“Wachezaji wa zamani wakati tunacheza soka tulikuwa tunacheza mpira kwa mapenzi na kujituma mno tukiwa uwanjani kulinganisha na wachezaji wa sasa japokuwa wakati huo tulikuwa hatupati fedha nyingi kama wanazopata wachezaji wa hivi sasa.

“Nakumbuka kabla ya kuanza kwa mazoezi kwanza tulikuwa tunafanya mazoezi binafsi kabla ya kocha hajafika na akifika tunaanza upya kwa kufuata programu yake ya siku hiyo aliyopanga.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles