Pep Guardiola awapa ubingwa Liverpool

0
784

Manchester, England

BAADA ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Manchester City kukubali kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Norwich City mwishoni mwa wiki iliopita kwenye michuano ya Ligi Kuu England, kocha wa timu hiyo Pep Guardiola amedai kichapo hicho kinawapa nafasi Liverpool kutwaa ubingwa msimu huu.

Guardiola amedai wapinzani wake Liverpool wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, hivyo anawapa pongezi kutokana na kuanza msimu vizuri kwa kushinda michezo yote mitano tangu kuanza kwa msimu huku Man City wakishinda michezo mitatu, sare mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja.

Kutokana na hali hiyo Guardiola amesema huu ni wakati wa Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kutokana na ubora wao.

“Tupo mwezi wa tisa, tutahakikisha tunapambana kuwa sawa baada ya kuanza vibaya, lakini niwapongeze wapinzani Liverpool naweza kusema wao ni mabingwa sasa, sisi hatupo vizuri ila tunajipanga.

“Hadi sasa tumepoteza pointi tano, nadhani mchezo dhidi ya Norwich City wachezaji wangu kutakuwa na kitu ambacho wamejifunza kwa ajili ya michezo ijayo,” alisema kocha huyo.

Kocha huyo amesema timu yake imeanza vibaya msimu huu kutokana na kuwa na wachezaji wengi majeruhi katika safu ya ulinzi, lakini baada ya muda watarudi katika ubora wao na kupambana kutetea taji hilo.

“Majeruhi yanawatesa wachezaji wangu na ndio maana timu haijaonekana kuwa sawa. Hata hivyo wachezaji waliopo walitakiwa kutumia nafasi hii kuonesha uwezo wao, lakini wanashindwa kufanya hivyo.

“Ninaamini kila mmoja akitekeleza majukumu yake kila kitu kitakuwa sawa, lakini niwe mkweli bila ya kufanya hivyo hali itakuwa ngumu kwa upande wetu msimu huu,” alisema Guardiola.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here