31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Pengo la Godzilla kwenye ‘Free Style’ halizibiki

NA BADI MCHOMOLO

FEBRUARI 16, mwaka huu, nyota wa muziki wa hip hop na mitindo huru ‘Freestyle’ nchini, Golden Jacob maarufu kwa jina la Godzilla, alilazwa kwenye nyumba yake ya milele baada ya kupoteza maisha  Februari 13, mwaka huu nyumbani kwake Salasala jijini Dar es Salaam.

Kifo hicho kiliwashtua wengi kwa kuwa wengi wao hawakuwa na taarifa juu ya kuugua kwake, lakini alipata maradhi ya siku chache na kupoteza maisha huku akidaiwa kusumbuliwa na malaria na sukari ya kushuka.

Msanii huyo ambaye amepoteza maisha huku akiwa na umri wa miaka 31, alikuwa na ushawishi mkubwa kwenye muziki wa hip hop pamoja na mitindo huru.

Ikumbukwe miaka saba au nane iliyopita, msanii huyo jina lake lilianza kujulikana kutokana na mashindano ya mitindo huru, ikiwa na maana ya kuimba mistari bila ya kuandika au kuirekodi.

Katika mashindano ambayo yaliandaliwa na kipindi cha Bongo Fleva cha Clouds FM chini ya mtangazaji wa enzi hizo, DJ Fetty, mshindi wa kwanza alitambulika kwa jina la Jackosn, huku Godzilla akishika nafasi ya pili na Nikki Mbishi akishika nafasi ya tatu.

Hata hivyo, mbali na Jackson kushika nafasi ya kwanza, hakuweza kuendelea na muziki wake kwa kurekodi nyimbo kama ilivyo kwa Godzilla na Nikki Mbishi, Jackson aliishia kwenye mitindo huru lakini Nikki na Godzilla waliendelea kuonesha ubora zaidi.

Aina ya uimbaji wa Godzilla pamoja na ile aina yake ya mitindo huru, aliweza kujizolea idadi kubwa ya mashabiki huku akidaiwa kuwa na mitindo ambayo inawavutia wengi (swaga).

Baada ya kushika nafasi ya pili, alionekana hana tena mshindani kwenye mitindo huru, hivyo aliamua kujikita moja kwa moja kwenye muziki na kufanikiwa kufanya nyimbo mbalimbali ambazo ziliweza kumtambulisha zaidi na kuwa mmoja kati ya wasanii wenye ushawishi.

Baadhi ya nyimbo ambazo alizifanya na kumuongezea idadi kubwa ya mashabiki ni pamoja na Lakuchumpa, King Zilla, Salasala, Milele, Nataka, Stay, First Class, Get High, Thanks God, Mama I Made it na nyingine nyingi.

Aina yake ya uimbaji ilikuwa inafananishwa na rapa wa Marekani, Curtis James Jackson 111 maarufu kwa jina la 50 Cent.

Aina ya uimbaji wa 50 Cent wa kubana meno wakati anaimba ulitokana na msanii huyo baada ya kupigwa risasi, lakini Godzilla aliweza kufanana nayo.

Kutokana na kupendwa na watu wengi, akatokea msanii mwingine nchini miaka michache iliyopita na kujulikana kwa jina la Bill Nas, hivyo ujio wake ulionekana wazi kuja kumpoteza Godzilla kwa kuwa wanafanana aina ya uimbaji.

Lakini hakuna ambaye angeweza kuvaa kiatu cha Godzilla, kila msanii ana aina na uwezo wake wa uimbaji, Bill Nas asingeweza kumfikia msanii huyo hata kama ameondoka.

kwa upande mwingine, kuondoka kwa Godzilla kunazidi kupoteza utamu wa mitindo huru, awali alikuwepo Albert Mangwea maarufu kwa jina la Ngwea, alitajwa kuwa mkali wa aina hiyo ya uimbaji, lakini alipoteza maisha Mei 28 nchini Afrika Kusini.

Pengo la Ngwea lilionekana kuwa kubwa kwenye muziki wa Bongo Fleva pamoja na mitindo huru na sasa kuondoka kwa Godzilla kunazidi kuufanya muziki huo uonekana unapoteza mastaa wao.

Bado wasanii ni wengi ambao wanafanya vizuri kwenye mitindo huru na hapo ndipo wanaweza kutumia nafasi vizuri ya kujitambulisha kwa mashabiki.

Tayari Godzilla aliweza kuutambulisha Mtaa wa Salasala uliopo maeneo ya Mbezi jijini Dar es Salaam, katika baadhi ya nyimbo zake alionekana kuutaja mtaa huo ambako ametokea katika maisha yake.

Hii ni kwa wasanii wengi wakubwa wamekuwa wakifanya hivyo hapa jijini kwa kuutambulisha mtaa ambao wametokea na kukulia, kama vile Nasibu Abduly ‘Diamond’ (Tandale-Sinza), Juma Nature (Temeke), Nyandu Tozi (Kinondoni), Chid Benz (Ilala), Ali Kiba (Kariakoo), Fid Q (Mwanza), Weusi (Arusha) na wengine wengi.

Kabla ya Godzilla kukutwa na umauti, alikuwa kwenye mipango ya kutaka kuachia video ambayo inaelezea maisha ya Salasala, hivyo aliwahi kusema kuwa kila kitu kimekamilika na kilichobaki ni muda uliopangwa kwa ajili ya kuachiwa, lakini hakuweza kufanya hivyo, amefariki kabla hatujaiona video hiyo ila si mbaya kwa kuwa tayari ameweza kuiwakilisha vizuri Salasala.

Godzilla alizaliwa Januri 5, 1988 huko mkoani Morogoro, baba yake alipoteza maisha huku Godzilla akiwa na umri wa miaka miwili.

Msanii huyo alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Neema Trust na baadaye akaja kupata elimu ya biashara katika Chuo cha Biashara (CBE) na hapo ndipo alipokutana na msanii Bill Nas.

Msanii huyo ameacha mtoto mmoja aitwaye Shwan mwenye umri wa miaka minne. 

Nenda Godzilla, umewaachia wakati mgumu wasanii kuibakisha mitindo huru kwenye ramani ya muziki wa Bongo Fleva na hip hop

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles