Na Elias Msuya, Dar es Salaam
IKIWA imebaki miezi 10 kufikia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka Watanzania walio masikini kuungana ili kuwang’oa madarakani viongozi matajiri wasiojali maslahi ya taifa.
Alisema kwa muda mrefu Watanzania wanafikiria ulimwengu utabadilishwa na watu wenye mabilioni na walio na fedha za Escrow jambo ambalo si sahihi.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya ibada ya sherehe za kutimiza miaka 70 ya kuzaliwa kwake iliyofanyika katika Kanisa la St. Joseph ambapo alisema kwa hali ya sasa ya Tanzania, mabadiliko lazima yatokee.
“Kwa muda mrefu sana Watanzania na labda siyo Watanzania ila kwa dunia kwa ujumla, tunafikiria ulimwengu utabadilishwa na watu wenye mabilioni, walio na fedha za Escrow, sijui na vitu gani, kwamba hao ndio watakaoleta mabadiliko. Hapo tunadanganyana sana,” alisema Kardinali Pengo na kuongeza:
“Wewe fikiria sisi Watanzania wengi tulio masikini, tungesema tumechoka na hali hii ya nchi, hao wenye madaraka hata wangekuja na mabomu, bunduki au fedha, sisi tukakubaliana kwamba hatuhongwi na mtu yeyote mwenye hela, mnaonaje, si tungeleta mabadiliko? Hivi ndivyo Mungu aliwaambia wachungaji.”
Huku akitoa mfano wa maandiko ya Biblia, Kardinali Pengo alisema Watanzania kwa sasa ni sawa na wachungaji wa mifugo wa wakati ule wa kuzaliwa Yesu, ambao waliletewa taarifa na malaika.
“Wakati ule malaika alipeleka habari njema kwa watu duni kabisa, wale wachungaji walikuwa ni watu ambao hakuna anayewahesabu wakati ule. Sasa malaika akawaambia nawaletea habari njema, amezaliwa Masiha. Katika kuwapa habari njema aliwapa ili wakawaambie watu wengine.
“Msiseme sisi wachungaji hawatatusikiliza, ni mimi au ni sisi kama tungekubaliana wenye fedha wangetuchangia na wakatupatia ingekuwa rahisi, lakini isingekuwa rahisi kwa ulimwengu huu. Walioneemeka wenye kipato kizuri, daima walikuwa na tabia ya kutunza kipato chao wabaki vilevile huku sisi wengi masikini tubaki hivyo hivyo,” alisema Kardinali Pengo.
Kiongozi huyo wa juu wa Kanisa Katoliki nchini, alishangazwa na jinsi Watanzania wengi walio katika hali ya umasikini lakini hawashtuki, huku akiahidi kuendelea kupaza sauti yake hadi waelewe.
“Kama Yohana Mbatizaji, nitapiga kelele nyikani, hata watu wasiponisikiliza, hata mawe yatanisikiliza na hayo yataleta mabadiliko… Najua Tanzania tuna wakati mgumu sana, lakini asiwepo hata mtu mmoja anayesema anakata tamaa kwa sababu mwingine amefanya hivi. Kila mmoja wetu atekeleze jukumu lake,” alisema.
Alisema katika nchi ni lazima yatokee mabadiliko ili kuleta utengamano kati ya masikini na matajiri na alisisitiza kuwa mabadiliko hayo yatakuja kama masikini na matajiri watakapokubaliana.
“Pengo la kipato kwa walionacho na wasionacho linakuja kutokana na wenye kipato kikubwa kuzidi kujilimbikizia… utajiri wa dunia una kikomo, tukiwa wengi wenye kipato, kwa kadiri kinavyozidi kuwa kikubwa ndiyo minofu inazidi kuwa mikubwa halafu tembo anamalizikia. Lakini mkiwa watu 100 na nyama ya tembo vipande vinakuwa vidogo, wale wenye njaa kama ya simba hawawezi kuridhika,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema pamoja na siasa kuwa ni moja ya njia zinazotumika ili kukuza nafasi ya mtu, jina na mapato ndiyo inayotengeneza mazingira yanayonusuru uchumi na jamii, ambapo siasa za Tanzania zinawasaidia wachache.
“ Ni lazima tuunganike na tusianze kutofautiana, utakuta masikini wanatofautiana, wewe sijui ni Mwislamu, wewe Mkristo, wewe sijui Mngoni wewe nani, unakuta tena umasikini unatutenganisha badala ya kutuunganisha. Hata mtakapoingia kwenye familia mtasema, huyu mrefu huyu sijui Mungu amemuumbaje, tofauti hazitatuunganisha,” alisisitiza.
Akizungumza katika ibada hiyo, Kardinali Pengo alisema anamshukuru Mungu kwa kufikia umri huo akisema ni upendeleo aliopewa na Mungu.
Kauli hiyo ya kiongozi huyo wa juu wa Kanisa Katoliki nchini imekuja siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete amfute kazi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka Desemba 22, mwaka huu alipokuwa akihutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Uamuzi huo wa Rais Kikwete ulikuja baada ya Bunge kupitia maazimio manane kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wa waziri huyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredereck Werema ambaye alijizulu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ambaye tayari amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake.
Awali akieleza lengo la ibada hiyo, Askofu Mkuu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Titus Mdoe, alisema Kardinali Pengo alitimiza umri wa miaka 70 Agosti 5, mwaka huu, lakini hali yake ya afya haikuwa nzuri ndiyo maana sherehe hizo zikaahirishwa hadi juzi.
“Kardinali amepewa zawadi ya miaka 70 iliyopita, anaifanyia kazi. Kuna kitu kimefanyika kwake yeye kama wakili na mtumishi wake. Anapojiweka mbele za Bwana ana kitu cha kusema,” alisema Askofu Mdoe.
Licha ya kusherehekea miaka hiyo, Askofu Mdoe alisema Kardinali Pengo anaadhimisha miaka 30 ya uaskofu wake na miaka 43 tangu alipopewa daraja la upadre.
“Miaka 30 ya uaskofu siyo michache… basi Mungu yumo ndani alimkabidhi mtu mwingine kuwa askofu wa jimbo kule Nachingwea. 1994 kuwa askofu siyo Dar es Salaam tu, bali majimbo yote. Mwaka 1998 akawa kardinali, kuwa mkuu siyo Tanzania tu bali Afrika na Madagascar na pia awe msaidizi wa Papa,” alisema Askofu Mdoe.