BAADA ya Manchester City kupokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Everton katika michuano ya Kombe la Capital One hatua ya nusu fainali, kocha Manuel Pellegrini, amemtupia lawama mwamuzi wa mchezo huo, Bobby Madley.
Mchezo huo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Goodison Park, ambayo ni nusu fainali ya kwanza, Pellegrini amedai kwamba Everton walibebwa kwa kiasi kikubwa.
Pellegrini amesema mwamuzi wa kati, Bobby Madley na wasaidizi wake walishindwa kuumiliki mchezo huo hasa katika bao la kwanza ambalo lilifungwa na Romelu Lukaku.
“Nimechukizwa sana na matokeo hayo, kwa kuwa hauwezi kuwa na furaha wakati umepoteza mchezo lakini ninaamini hatukustahili kupoteza mchezo huo kwa kuwa bao lao la kwanza lilikuwa wazi ni lakuotea.
“Lukaku alikuwa mbele kabisa bila beki yeyote, lakini ninashangaa kuona waamuzi wakiwa kimya wakati ilikuwa wazi kwamba Lukaku ameotea, kila mtu aliliona hilo.
“Hata hivyo, tulistahili kupata penalti baada ya Jesus Navas kuchezewa vibaya katika eneo la hatari, lakini kikubwa ni kujipanga na mchezo ujao tukiwa nyumbani ili kuhakikisha tunasonga mbele,” alisema Pellegrini.