Paul Pogba aanza safari kuelekea United

Paul PogbaLOS ANGELES, MAREKANI

KIUNGO wa klabu ya Juventus, Paul Pogba, ameanza safari yake kutoka jijini Los Angeles nchini Marekani na kuelekea jijini Manchester kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na mashetani wekundu, Manchester United.

Mchezaji huyo amekuwa akisubiriwa kwa muda mrefu kuweza kukamilisha usajili huo ambao unadaiwa kuwa utavunja rekodi ya usajili duniani, lakini inadaiwa kwamba muda wowote kuanzia sasa atakuwa anamalizana na klabu hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, anatarajia kumalizana na klabu hiyo kwa kitita cha pauni milioni 100 na kutaka kufunika usajili ambao unaonekana kuwa wa fedha nyingi wa Gareth Bale wa kujiunga na klabu ya Real Madrid akitokea klabu ya Tottenham kwa kitita cha pauni milioni 86.

Uhamisho wa Bale ni usajili wa pekee ambao umetikisa duniani na kudaiwa kuwa ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimetumika, lakini huu wa Pogba unataka kuvunja rekodi za usajili duniani.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Pogba ameweka picha yake ambayo inamuonesha akitokea jijini Los Angeles na kuelekea jijini Manchester na kuandika kwamba ‘Mungu ni mkubwa’.

Hii ni ishara tosha ya kuwaonesha mashabiki wa Manchester United kuwa tayari amekubaliana na uongozi wa klabu hiyo, kilichobaki ni kuuweka wazi usajili wake.

Hata hivyo, mchezaji huyo aliandika kwamba safari yake ilichelewa kutokana na masuala hayo ya michezo, lakini kwa sasa kila kitu kipo sawa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here