26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

PATRICK BALISIDYA ANAENDELEA KUISHI KUPITIA TUNGO ZAKE

 

NA VALERY KIYUNGU

KARIBUNI kwa mara nyingine wasomaji wa safu hii muipendayo, ambayo pamoja na mambo mengine, inawaletea simulizi za wanamuziki wa zamani waliowahi kufanya vizuri miaka mingi iliyopita, ambao wengine mpaka sasa wanaendelea kufanya sanaa.

Kwenye Old Skul leo tunakuletea simulizi ya Patrick Balisidya, ambaye enzi za uhai wake alikuwa mwanamuziki wa dansi akiwa kama mtunzi, mwimbaji, mpiga gitaa la solo, kiufupi alikuwa ni mwanamuziki aliyekamilika.

Mkongwe huyo wa muziki wa Dansi alifariki miaka 13 iliyopita na akazikwa kwenye makaburi ya Buguruni Malapa, jijini Dar es Salaam siku kama ya leo, yaani Agosti 12 mwaka 2004.

Mwanamuziki huyu jina lake halisi ni Patrick Pama Balisidya, alizaliwa Aprili 18, mwaka 1946, maeneo ya Mvumi, mkoani Dodoma, kabila lake ni Mgogo.

Suala la muziki limeonekana kuwa ndani ya damu yake, hasa ikizingatiwa kuwa mama yake alikuwa mpiga kinanda katika kanisa moja lililopo Dodoma, hivyo alitokea kuupenda muziki akiwa bado mdogo.

Kupenda kwake muziki kulidhihirisha wakati alipokuwa anasoma katika Shule ya Sekondari Dodoma, ambapo alikuwa  kiongozi wa bendi ya shule, chini ya uongozi wake iliweza kufanya vizuri kwenye sherehe mbalimbali ilizokuwa inatumbuiza.

Patrick baada ya kumaliza masomo katika shule hiyo ya sekondari, baadaye alijiunga na chuo kimoja cha ufundi kwa lengo la kujiendeleza zaidi, ambapo baada ya kumaliza alifanya kazi ya ufundi kwa muda mfupi, kabla ya kurudi tena kwenye muziki.

Kuanza muziki

Baada ya kuacha kazi ya ufundi alianza kusaka bendi, ambapo bendi ya kwanza kujiunga nayo ilikuwa ni Dar es Salaam Jazz, maarufu ‘Majini wa Bahari’, ambapo hata hivyo hakuweza kudumu nayo kwa muda mrefu na baadaye akaondoka.

Alipata wazo la kuwa na bendi yake, ndipo mwaka 1970 alianzisha bendi ya Afro 70, ikiwa inatumia mtindo wa Afrosa.

Balisidya akiwa na bendi ya Afro 70 mnamo mwaka 1977, aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Tanzania katika maonyesho ya Mtu Mweusi (FESTAC Festival 1977), yaliyofanyika katika Jiji la Lagos, nchini Nigeria.

Kadhalika enzi za uhai wake mwanamuziki huyo alifanya juhudi za muziki, katika kuhakikisha anaendeleza kipaji chake mwaka 1979, alisafiri hadi nchini Sweden kufanya shughuli za muziki.

Old Skul inamkumbuka Patrick kwa kazi yake nzuri katika tasnia ya muziki wa dansi, hususan pale alipojiunga na bendi ya Orchestra Safari Sound (Masantula), ambapo alionyesha uwezo wa hali ya juu katika upigaji wa piano katika wimbo unaoitwa Unambie Siri.

Patrick pia alikuwa mpigaji mahiri wa kinanda, huku akibobea katika kutunga nyimbo zenye maudhui mbalimbali na nyimbo alizowahi kuzifanya ni kama vile Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa, Nakupenda kama lulu, Ni Mashaka, Mahangaiko na Afrika, ambapo hadi sasa zipigwapo hudhaniwa kuwa ni mpya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles