22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

PASAKA IWAKUMBUSHE VIONGOZI HEKIMA

 

Na TOBIAS NSUNGWE,

BILA shaka yapo maandiko mengi yameandika kuhusu siku hii ya leo ambayo Watanzania wanaungana na Wakristu wenzao duniani kote kukumbuka kufufuka kwa Bwana Yesu Kristu, zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Mwezi huu Taifa letu limekumbuka pia mambo makuu matatu. Kwanza, Aprili 7, mwaka huu Taifa lilifanya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Jumatano iliyopita kulikuwa na  kumbukizi ya miaka 33 tangu kutokea kifo cha Waziri Mkuu, Edward Sokoine.  

Aprili 13, mwaka huu ilifanyika kumbukumbu ya miaka 95 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Katika mdahalo wa kumkumbuka mwasisi huyo wa Taifa, wazee wetu wastaafu, akiwamo Joseph Butiku, walitukumbusha msingi mkuu aliotuachia Mwalimu Nyerere, yaani: “Binadamu wote ni sawa”.

Sikukuu hii ya Pasaka inasisitiza upendo, kwani hata Bwana Yesu alipofufuka aliwaambia wafuasi wake: “Amri mpya nawapa. Mpendane. Nasi Watanzania tunaposherehekea sikukuu hii tujikumbushe wajibu wetu wa kupendana bila kujali rangi, kabila, dini, itikadi au hali ya uchumi ya jirani au majirani zetu.

Siku hizi imezuka tabia ya kuyatumia makanisa kama biashara na vijiwe vya kusengenyana au kupitishia bidhaa haramu. Pasaka itukumbushe wajibu wetu wa kupambana na shetani anayetumia mdudu fedha kuyaharibu makanisa. Mara kadhaa kumeibuka mizozo katika baadhi ya makanisa, waumini wakigombea sadaka na mali za kanisa.

Nawakumbusha wanajumuia ndogondogo wa Kanisa Katoliki kudumisha upendo. Pasaka iwasaidie waumini kutotumia jumuia hizo kuchunguzana au kusengenyana. Waumini wajenge utamaduni wa kusaidia watu wote, hasa masikini. Wasishabikie waumini wenye uwezo tu.

Wanajumuia washiriki maziko ya kila muumini bila kujali aliishi namna gani hapa duniani.

Si busara kwa waamini kukataa kuzikana Kikristo eti kwa kuwa aliyefariki alikuwa hahudhurii kanisani au kwenye jumuia. Pasaka itukumbushe kuacha tabia ya kuhukumu. Ili mradi ndugu wamethibitisha kwamba marehemu alikuwa Mkatoliki basi azikwe kwa heshima zote za Kikatoliki. Makatekista waache kuzihukumu maiti. Kazi hiyo wamwachie Mola, kwani yeye ndiye anajua marehemu aliishi vipi hapa duniani.

Pasaka hii pia iwakumbushe masheikhe, mapadri na maaskofu wajibu wao wa kuhudumia watu wa aina zote, iwe kwenye mazishi, hitima, maulidi, harusi au kipaimara.

Nasema si busara kwa viongozi wa dini kujiweka mbele sana kutoa huduma kwa viongozi wa Serikali na wafanyabiashara wakubwa, lakini kuwa wagumu kushiriki shughuli za ‘watu wa kawaida’. Sikukuu hii iwakumbushe mababa zetu wa kiroho kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu watu wote ni sawa.

Kazi ya viongozi wetu wa dini iwe ni kuwafikia wanyonge ili kuwasaidia kujikomboa katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kifikra.

Pasaka hii iwamulike baadhi ya viongozi wa dini ambao kazi yao ni kujikomba kwa wanasiasa. Sikukuu hii ije na baraka za kuwasaidia waimbaji, makatekista, mapadri, masheikhe, wachungaji na maaskofu kuishi maisha nyoofu ili waendelee kuwa kioo kwa waumini.

Pasaka ije na baraka za kuwawezesha wazazi kuwa mfano bora kwa watoto wao. Si vizuri kwa wazazi kugombana au kujibizana mbele ya watoto. Yesu mfufuka aziponye ndoa zinazougua hata zile zinazoelekea kufa, umasikini, chuki na dharau.

Wanazuoni wanasema binadamu ni moja ya viumbe wakatili zaidi. Hata hivyo, tabia ya ukatili kwa binadamu inapunguzwa kwa kupata elimu dunia na zaidi elimu ya dini ambayo inahimiza upendo.

Sasa ni wakati wa Watanzania kuachana na tabia ya kujichukulia sheria mkononi. Mtanzania ninayejiita Mkristo sitarajiwi kumuua mwizi  au kibaka kwa sababu yoyote ile, hata kama ameniibia mimi!

Mwizi au mhalifu yeyote anatakiwa kukamatwa na kupelekwa polisi, hatimaye mahakamani. Pasaka ya mwaka huu iwape Watanzania neema ya kujali utu.

Kundi moja la waumini watakaojitokeza kutoa sadaka kwenye misa ya Sikukuu ya leo ni watumishi waandamizi katika sekta ya umma. Wajiridhishe kama fedha wanazotoa wamezipata kwa njia halali zisiwe za rushwa au hongo. Wizi wa mali ya umma ni dhambi, kwani unaikwamisha Serikali kutoa huduma ambazo zingewafikia Watanzania wote.

Nawakumbusha tena wananchi kutohalalisha matumizi mabaya ya mali za umma kwa kuwaita “wajanja” wezi wa mali hizo, hasa pale wanapozitumia kwa kujenga nyumba za kifahari na au kuchangia fedha nyingi kwenye miradi ya makanisa.

Idadi kubwa ya viongozi wetu wa kisiasa hujipambanua kwamba wao ni wacha Mungu na humtaja mara kwa mara. Pasaka hii iwape neema viongozi wetu wa kitaifa kuongoza kwa hekima na busara, kwani wamepewa madaraka makubwa.

Pengine jambo kubwa sana la kuomba baraka za Pasaka, hii ni kuwaepusha viongozi na balaa la kulewa madaraka. Kiongozi akilewa madaraka hujaa kiburi, haambiliki, hashauriki na hujifanya haoni japo ana macho.

Matukio yaliyojitokeza hivi karibuni ya polisi kuuawa na majambazi, mbunge kutishiwa baistola, wasanii kutekwa na lile la uvamizi wa redio na watu wenye silaha ni viashiria kwamba nchi yetu imetikiswa.

Matukio kama hayo yanasababisha watu kuacha kujadili mambo mengine, ikiwamo Bunge la Bajeti, tafakari ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere, ukame au ugomvi wa wakulima na wafugaji.

Tanzania sasa ni kama koti. Pasaka hii ije kama sabuni kulisafisha koti hili, kwani matukio yaliyotokea hivi karibuni yamelipaka matope.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles