TAMASHA la Karibu Music Festival 2015, litazinduliwa Novemba 6 hadi 8 mwaka huu katika viwanja vya Mwanakalenge, Bagamoyo, huku mwanamuziki kutoka Congo, Papa Wemba, akitarajiwa kulinogesha.
Katika Tamasha hilo lenye lengo la kukuza muziki wa Afrika, wasanii wa bongo fleva, wasanii na vikundi vya ngoma na nyimbo za asili watatumbuiza, lakini pia warsha za mafunzo mbalimbali kuhusu sanaa zitaendeshwa.
Baadhi ya wasanii wanaotarajiwa kutoa burudani ya kutosha katika siku tatu za tamasha hilo ni pamoja na mkali wa nyimbo za reggae nchini, Jhikolabwino Manyika (Jhikoman), Misoji Mkwabi, aliyewahi kuwa mshindi katika shindano la Bongo Star Search (BSS) na kiongozi wa kundi la Wanaume Halisi, Juma Kassim ‘Juma Nature’.
Wengine ni msanii anayeimba na kupiga ala za asili, Msafiri Zawose, The Spirity Band ambayo anaimba Nassibu Fonabo, aliyekuwa mshindi wa pili wa BSS mwaka 2015 na wengine wengi wa ndani na nje ya nchi.
Tamasha hilo la Karibu Festival kwa mwaka huu linafanyika kwa mwaka wa pili, likiwa limeboreshwa vema baada ya mara ya kwanza kukumbwa na changamoto za mvua zilizokuwa zikiendelea ambazo zilisababisha kusimamishwa kwa onyesho mara kwa mara kutokana na jukwaa kuu kutokuzibwa juu.