29.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Papa abariki kwa Kiswahili

POPE8NAIROBI, KENYA

KIONGOZI wa Kanisa la Katoliki Duniani, Papa Francis, amewasili nchini Kenya jana jioni huku akitoa baraka kwa nchi hiyo kwa lugha ya Kiswahili.

Baada ya hotuba yake, Papa Francis, alimaliza kwa kusema “Mungu Ibariki Kenya” jambo lililowafanya watu waliokuwa katika ukumbi wa Ikulu ya Nairobi kulipuka kwa furaha.

Katika ziara yake hiyo ya ya siku tatu nchini Kenya, alipokewa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, ambapo moja ya mambo ya kukumbukwa ni ujumbe alioutoa kwa Kiswahili akilibariki taifa hilo baada ya kulihutubia taifa Ikulu jijini Nairobi.

Pamoja na mambo mengine, alisisitiza umuhimu wa amani, maridhiano, kusameheana na uponyaji katika taifa hilo lililogawanyika kwa misingi ya ukabila.

 

PAPA AHUTUBIA TAIFA

Baada ya mazungumzo yao Ikulu, Rais Kenyatta akagusia kwamba leo ni siku ya maombi ya taifa la Kenya na baadaye akamkaribisha Papa Francis kulihutubia taifa.

Papa alianza kutoa hotuba akishukuru kwa makaribisho mema kwenye ziara yake ya kwanza Afrika.

Kuhusu matarajio ya ziara yake, Papa alisema Kenya ina vijana wengi, na hivyo katika siku zake za kuwa humo anasubiri kwa hamu kubwa kukutana na kuzungumza nao na kuwapa matumaini katika ndoto zao za siku za usoni.

Aidha alisema Kenya ni taifa change, linalokua na lenye jamii mseto na ambalo limekuwa likitekeleza jukumu muhimu katika kanda hii na kupitia changamoto nyingi katika uundaji wa demokrasia kama ilivyo kwa mataifa mengi Afrika.

Akihimiza amani na maridhiano Papa Francis alisema: “Jamii zetu zinapoendelea kukumbwa na migawanyiko ya kikabila, kidini au kiuchumi, binadamu wote wenye nia njema huitwa kufanyia kazi maridhiano, msamaha na uponyaji.

“Yote ni katika juhudi za kuunda mfumo wa demokrasia, kuimarisha utangamano na uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana, lengo kutenda mema linapaswa kuwa kipaumbele kikuu.”

Aidha alisema kwamba historia inaonyesha kuwa ghasia, mizozo na ugaidi huchochewa na kuogopana na kutoaminiana ambako husababishwa na umaskini na kupoteza matumaini.

“Vita dhidi ya maadui wa amani na ustawi vinapaswa kuendeshwa na wanaume na wanawake wanaoamini katika kushadadia, maadili makuu ya kidini na kisiasa ambayo yalisababisha kuasisiwa kwa taifa,” alisema.

Akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira, Papa Francis alisema: “Kenya imebarikiwa si tu na umaridadi, katika milima, mito na maziwa, misitu, nyika na maeneo kame, bali pia katika utajiri wa maliasili.

“Wakenya wamethamini zawadi hizi kutoka kwa Mungu na wanajulikana kwa utamaduni wao wa kuhifadhi mazingira. Mgogoro wa kimazingira unaoikumba dunia kwa sasa unahitaji kutambua zaidi uhusiano kati ya binadamu na maumbile.”

Alihimiza taifa kuwajali masikini, ndoto za vijana, na kugawana vyema maliasili na nguvu kazi ambazo Mungu ameibariki Kenya na ameahidi kuendelea kwa juhudi za Kanisa Katoliki, kupitia kazi zake za elimu na kusaidia jamii, kutoa mchango katika hilo.

Akimalizia hotuba yake kabla ya kuondoka katika ukumbi wa Ikulu, baada ya kusalimiana na baadhi ya wageni waalikwa alisema: “Nawashukuru tena kwa kunikaribisha vyema, na kwenu na familia zenu, na watu wote wa Kenya, ziwe baraka tele za Mwenyezi Mungu.” Kisha akamalizia kwa Kiswahili akisema: “Mungu Ibariki Kenya”.

Baada ya hotuba hiyo, Papa alikaribishwa katika dhifa ya kitaifa iliyofanyika katika hema kubwa la mviringo eneo la Milimani, Nairobi, ambako ni makazi ya rais na ofisi yake.

 

NDEGE ILIYOMBEBA

 

Awali ndege iliyombeba Papa ya Shirika la Ndege la Italia, Alitalia, ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa 10. 33 jioni.

Viongozi wa Kanisa la Katoliki nchini humo, wanasiasa na mabalozi wakiongozwa na Rais Kenyatta walionekana wamejiandaa kumlaki.

Waandishi wa habari walioambatana na Papa walitangulia dakika 17 baadaye, kabla ya yeye mwenyewe kuchomoza kutoka katika ndege hiyo dakika mbili zilizofuata.

Papa alilakiwa kwa shangwe na nderemo huku kwaya ya kumkaribisha ikitumbuiza, na alianza kusalimiana na Rais Kenyatta kabla ya kutembezwa kutambulishwa na kushuhudia vikundi mbalimbali vya utamaduni.

Kwa mujibu wa Idara ya Habari ya Serikali ya Kenya, Papa Francis akiwa JKIA aliandika maneno haya: “Na maombi na shukrani kwa kuwatunza wasafiri.”

Papa baada ya kupokewa kwa heshima zote za kitaifa uwanjani hapo, msafara ulianza kuelekea Ikulu ya Nairobi ukipita mitaani, ambako maelfu ya Wakenya walijipanga pembeni mwa barabara kumsalimia, huku wengine wakipeperusha bendera na mabango ya kumkaribisha yakiwamo yenye picha yake.

 

APIGIWA MIZINGA

 

Alipokewa Ikulu na Rais Kenyatta, ambako wimbo wa taifa ulipigwa kabla ya mizinga 21 kupigwa kwa heshima yake kama mkuu wa taifa la Vatican.

Baadaye Papa Francis alikagua gwaride la heshima kabla ya kwenda kuonana na Rais Kenyatta na baadhi ya wageni waalikwa na baadaye kulihutubuia taifa akiwa Ikulu.

Rais Kenyatta pia alimtambulisha Papa kwa wajumbe wa baraza lake la mawaziri akiwamo naibu wake William Ruto kabla ya dhifa ya kitaifa aliyomwandalia.

Kabla ya mazungumzo Ikulu, Papa Francis, ambaye anajulikana kwa uhimizaji, utunzaji wa mazingira, pia alipanda mti akisaidiwa na Rais Kenyatta.

Mbele ya hema kulikuwa na kiti ambacho Papa alikaa pembeni ya Rais Kenyatta.

Wakati Papa akitarajia kukutana na watu wa kawaida wakati wa ziara yake Kangemi kesho na kukutana na vijana huko Kasarani, mkutano wake wa kwanza ulikuwa jana na tabaka la watawala na vigogo wa Kenya.

 

MARAIS WASTAAFU

 

Marais wastaafu Daniel arap Moi na Mwai Kibaki, Naibu Rais William Ruto na Mke wa Rais, Margaret Kenyatta walikuwapo viti vya mbele wakati wa dhifa ya taifa wakiwa mkabala na Papa na Rais Kenyatta.

Pembeni yao walikuwepo maspika Justin Muturi na Ekwee Ethuro na wake zao. Wengine katika mstari wa mbele walikuwepo Jaji Mkuu Willy Mutunga, Waziri wa Mambo ya Ndani Joseph Nkaissery, Makamu wa Rais wa zamani Moody Awori.

Wengine ni Musalia Mudavadi, Kiongozi wa Wachache katika Seneti Moses Wetang’ula, viongozi wa muungano wa Cord, Kalonzo Musyoka na Raila Odinga na mkewe Ida pia walitarajia kuhudhuria dhifa hiyo.

Majaji wa mahakama ya juu, wabunge, majaji na wengineo pia walitarajia kuwapo jana usiku.

Papa leo asubuhi anatarajia kuongoza ibada itakayohudhuriwa na watu milioni 1.4 kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Nairobi.

Awali kutokana na shauku ya kuwasili kwake nchini Kenya, mapema jana Papa Francis alirusha ujumbe wa baraka kwa Wakenya kwenye mtandao wa jamii.

 

PAPA ARUSHA UJUMBE KWA KISWAHILI

Katika ujumbe wake alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter, @Pontifex the Papa aliandika kwa Kiswahili na Kiingereza maneno: “Mungu Ibariki Kenya!”

Aliutuma ujumbe huo jana mchana wakati akiwa safarini kutoka Rome, Italia kuelekea Nairobi.

Papa pia atazuru Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ambayo imekumbwa na machafuko baina ya Wakristo na Waislamu.

“Naenda nikiwa na furaha ya kuonana na Wakenya, Waganda na ndugu zetu katika Afrika ya Kati,” aliwaambia waandishi wa habari katika ndege yake.

Pia alipuuza wasiwasi wa usalama wake kwa kutania: “Ninaogopa zaidi mbu kuliko vita.”

Nairobi, linakuwa jiji la kwanza la Afrika, ambalo Papa huyo mwenye umri wa miaka 78 ametua tangu akabidhiwe uongozi wa kanisa miaka miwili iliyopita.

Anaitumia ziara yake ya 11 nje ya makao makuu ya kanisa hilo, Vatican kutoa jumla ya hotuba 19 kuhusu amani, haki za kijamii, utunzaji wa mazingira na majadiliano ya imani tofauti nchini Kenya, Uganda na CAR.

 

WASIOMJUA MUNGU WAFUNGUA KESI

Wakati huo huo, muungano wa watu wasiotambua uwepo wa Mungu, umewasilisha malalamiko yao mahakamani kupinga hatua ya Serikali ya Kenya kuitangaza Alhamisi (leo) kuwa siku ya mapumziko ya taifa.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa muungano huo, Harrison Mumia, wanaitaka mahakama itupilie mbali tangazo lililochapishwa katika gazeti la Serikali kuwa Alhamisi itakuwa siku ya mapumziko.

Juzi Rais Uhuru Kenyatta aliweka bayana kuwa Novemba 26 (leo) iwe mapumziko ya taifa kwa kuomba na kumwabudu Mungu wakati wa ziara ya Papa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles