NA MWANDISHI WETU, Dar es Salaam
CHUO Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kimepata suluhisho la kupunguza kuzaliana panya nchini, kwa kuanzisha uzazi wa mpango kwa wanyama hao.
Akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana, Mtaalamu wa Kilimo wa Chuo hicho, Thoneson Mhamphi alisema, utafiti huo ambao upo katika hatua za awali haujaweza kusambazwa.
Mhamphi alisema dawa hizo za uzazi wa mpango zinazojulikana kama Quinestro na Levonorgester, zimekuwa zikichanganywa kwenye chakula na kuwapatia panya hao, hatua inayowafanya washindwe kuzaliana.
“Huu utafiti ndiyo tumeanza kuufanyia kazi hivi sasa na umeonyesha mafanikio kwa sababu baada ya kuwapa chakula hicho panya hao wameacha kuzaana,” alisema.
Alisema dawa hiyo husababisha panya dume kuwa na nguvu ndogo ya kuzalisha kwa vile kizazi cha jike hujaa maji.
Mtaalamu huyo alisema panya wana kasi ya kuzaliana ana anaweza kuzaa kila baada ya wiki tatu.
Vilevile, panya ana uwezo wa kupata mimba tena saa 24 baada ya kuzaa, alisema mtaalamu huyo.
Alisema utafiti huo unaendelea kufanyika katika hatua nyingine kuona jinsi ya kukabiliana na panya waliopo mashambani.
“Mlipuko wa panya ni mkubwa na kama tusipopata njia za kuwadhibiti, hali katika mashamba yetu inaweza kuwa mbaya kabisa,” alisema.