30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Panga la mwisho wenye vyeti feki

necta*Necta sasa yatangaza kuwafuata kwenye vituo vyao vya kazi

*Yatoa ratiba ya kupita mkoa kwa mkoa, itakagua cheti cha kidato cha nne, sita na ualimu

 

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

HATUA ya Baraza la Mitihani nchini (Necta) kutoa ratiba ya kufanya uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na ualimu kwa watumishi wote wa umma sasa ni wazi imezidi kupandisha joto kwa vigogo na watumishi mbalimbali ambao hawana sifa za kielimu kushika nafasi walizo nazo.

Katika taarifa yake ya sasa Baraza la Mitihani nchini, limetangaza kuwafuata katika maeneo yao ya kazi watumishi wote walioko katika mamlaka za mikoa, halmashauri na manispaa kwa ajili ya kufanya uhakiki wa vyeti vyao hivyo vya kitaaluma.

Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na  Edga Kasuga kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo kwenda kwa Makatibu tawala wa Mikoa, uhakiki utafanyika katika ofisi za Makatibu Tawala wa mikoa kuanzia Oktoba 10 hadi 14 mwaka huu, ingawa ratiba nyingine ya uhakiki imeonyesha zoezi hilo litafikia tamati Novemba 7 mwaka huu.

“Ili kufanikisha zoezi hilo Baraza limetaka kupata orodha (nakala- laini ya soft copy) ya watumishi wote wa umma waliopo katika mkoa, halmashauri na manispaa.

“Nakala za vyeti vya kidato cha nne, cha sita na ualimu vya watumishi wote walioandikishwa na chumba cha kufanyia uhakiki,” inaeleza taarifa hiyo ya Baraza la Mitihani.

 

RATIBA YA UHAKIKI

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani, uhakiki huo utafanywa katika makundi matano katika mikoa tofauti tofauti.

Oktoba 10, mwaka huu kundi la kwanza litafanya uhakiki katika Mkoa wa Mtwara, kundi la pili Singida, kundi la tatu Rukwa, kundi la nne Katavi na kundi la tano litakuwa Geita.

Oktoba 17 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Lindi, la pili Manyara la tatu Songwe, la nne Kigoma na la tano litakuwa Mwanza.

Oktoba 24 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Morogoro, la pili Arusha, la tatu Mbeya, la nne Tabora na la tano Mara.

Oktoba 31 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Pwani, la pili Kilimanjaro, tatu Ruvuma, la nne Shinyanga na la tano Simiyu.

Novemba 7 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Dar es Salaam, la pili Tanga, la tatu Njombe, la nne Dodoma na la tano Iringa.

 

JOTO LA UHAKIKI

Kabla Baraza la Mitihani halijatangaza ratiba hiyo, tayari watumishi wa umma ambao wanatumia majina matatu lakini vyeti vyao vya elimu vinasomeka majina mawili walikuwa wamepewa maelekezo ya kwenda kutafuta hati ya kiapo kwa ajili ya kuapa mahakamani ili kuthibitisha majina yao.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili mmoja wa watumishi hao alisema: “Wakati tunaanza kazi sisi ambao vyeti vyetu tulikuwa tunatumia majina mawili shuleni, tuliambiwa tutumie matatu ambayo pia yanatumika hata kwenye ‘salary slip’, sasa tumeambiwa tunatakiwa kwenda mahakamani kuthibitisha.”

Alisema zoezi hilo tayari limeleta changamoto kubwa mbali na kuzua hofu kwa baadhi ya watu ambao taarifa zao za kitaaluma hazipo sawa sawa.

“Mimi binafsi sina hofu zoezi linakwisha kesho lakini kinachoniuma ni kwamba hiyo hati ya kiapo (affidavit) tukienda Mahakama ya Mwanzo tunaambiwa ni lazima tulipie shilingi 10,000 na kibaya zaidi hatupewi risiti lakini kwa watumishi wengine ambao wanafahamiana wanapata huduma bure,”  alisema mtumishi huyo.

Tangu Serikali itangaze kuwafuatilia watumishi wake wote wenye vyeti feki hali ya wasiwasi na sintofahamu imetawala miongoni mwa vigogo, maofisa na watumishi wengine ambao vyeti vyao vya kitaaluma haviko sawa sawa au haviendani na kazi au nyadhifa wanazoshikilia.

Wasiwasi unaozungumzwa pia umeonekana wazi kupitia ongezeko la matangazo ya kupotelewa vyeti kwenye vyombo vya habari katika kipindi cha hivi karibuni.

Wakati fulani gazeti hili liliwahi kufanya uchunguzi na kubaini kuwa tangu Serikali itangaze vita na watu wenye vyeti feki kwa wastani vyombo vya habari hususani magazeti yalikuwa yakipokea wastani wa matangazo 50-100 ya watu wanaodai kupotelewa vyeti.

Si hilo tu, wakati fulani iliwahi kuripotiwa na vyombo vya habari kuwa

baadhi ya maofisa wanaoshikilia nafasi nyeti kwenye taasisi mbalimbali za umma wamekosa amani na kulazimika kutumia muda mwingi nje ya vituo vyao vya kazi kwa nia ya kutatua tatizo ambalo wanahisi litawakumba kutokana na utata wa vyeti vyao vya shule na taaluma mbalimbali walizodai kusomea.

Wakati wa Bunge la Bajeti ya 2016/2017 lililoketi miezi michache iliyopita, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema Serikali imedhamiria kuboresha kiwango cha elimu nchini na kwamba kuitaja hatua mojawapo inayochukuwa sasa ni kukagua uhalali wa vyeti vyote vya elimu kwa watumishi wote wa umma.

“Tumekubali kwamba tuna changamoto… katika changamoto hizi lazima tuwe na mahali pa kuanzia na hivyo tunapochukua hatua tunaomba Watanzania mtuunge mkono,” alikaririwa akisema Prof. Ndalichako.

Kauli hiyo ya Ndalichako ilikuja wakati Serikali ya Rais John Magufuli ikijiapiza kusafisha uozo iliodai kuukuta serikalini.

Tayari taasisi mbalimbali za umma zilitangaza kuwapo kwa uhakiki wa vyeti vya watumishi wao, mbali na halmashauri za wilaya, pia Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Hali hiyo inaelezwa kuzusha hofu miongoni mwa vigogo na watumishi wa umma ambao inaelezwa waliingia kazini kwa vyeti ambavyo si vyao au vya kufoji licha ya kujiendeleza wakati wakiwa kazini.

Awali kabla ya uamuzi wa sasa wa Necta, ilitangaza watu wote wanaojijua wazi kuwa wanamiliki vyeti bandia kujisalimisha wenyewe.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Charles Msonde, alitoa tangazo hilo miezi michache iliyopita akisema kuwa Necta ndiyo yenye dhamana ya kutoa vyeti vyote vya watahiniwa wanaomaliza mitihani ya Taifa nchini.

Dk. Msonde aliwahi kusema kwamba  kulikuwa na changamoto ya vyeti feki (bandia) kwa kipindi kirefu kiasi cha mwaka 2008 baraza hilo kufikia hatua ya kubadili utaratibu wa utoaji wa vyeti.

Utaratibu huo ni pamoja na kuwekwa picha ya mtahiniwa.

Dk. Msonde aliwahi kukaririwa na gazeti hili akiwataka wale wanaojijua kuwa wanamiliki vyeti feki na wanavitumia kuombea nafasi mbalimbali za kazi wajitokeze na kujisalimisha vinginevyo watawakamata na sheria itachukua mkondo wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles