33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

‘Padri Pekupeku’ anayemiliki shule chakavu, kufaulisha vizuri

RICCARDO1Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

ALFA Gems ni shule ya sekondari inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro Mjini, ikiwa chini ya usimamizi wa Padri Riccardo Riccioni (65).

Umaarufu wa shule hiyo iliyopo katika Kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro Mjini, unatokana na Meneja wa shule hiyo, Padri Riccion, maarufu kwa jina la Padri Pekupeku.

Padri huyo amekuwa akisimamia shule hiyo kikamilifu kwa misingi ya kitaaluma, maadili na malezi bora ya kiroho.

Umaarufu mwingine wa shule hiyo unachangiwa na matokeo mazuri ya wanafunzi ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007.

Mazingira magumu yaliyopo shuleni hapo na ufaulu mzuri kwa wanafunzi unamsukuma mwandishi wa makala haya kufika ili kujua siri zaidi ya mfanikio.

Majengo mengi ya shule hiyo ni chakavu ambapo milango na madirisha ya madarasa imeshambuliwa na mchwa kiasi cha kuwafanya wanafunzi kusoma katika mazingira magumu.

Katika ofisi ya meneja wa shule hiyo kulikuwa na kiti kimoja tu ambacho hukalia mwenyewe.

Ilipofika saa 6:15 mchana, Padri Roccioni alionekana kwa mbali akitoka katika moja ya darasa ambalo mlango wake ulikuwa umeegeshwa upande baada ya kung’oka.

Alipofika katika eneo tulipokaa wageni mbalimbali tukisubiri kupata huduma aliuliza wanaotaka kuingia na kuwakaribisha, ndipo mazungumzo yangu na yeye yakaanza.

Bila kujali nafasi ya mgeni aliyekuja, mavazi yake yanaonyesha kuwa ni mtu anayependa kuishi maisha ya kifukara na kwa mtu asiyemjua anaweza kupata mshangao juu ya maisha ya padri huyo.

Padri Riccioni: Karibu sana.

Mtanzania: Ahsante.

Padri Riccioni: Samahani ofisi yangu haina viti ngoja tuombe nafasi kwa kaimu mkuu wa shule tuweze kuongea.

Mtanzania: Tueleze historia yako na na siri ya shule yako kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

Padri Riccioni: Kwa mara ya kwanza nilifika nchini mwaka 1984 katika Mkoa wa Iringa nikitokea nchini Italia nikiwa na Shirika Fransiscani la ndugu Wadogo.

Safari yangu ya utume ilianzia katika jimbo la Iringa katika Kijiji cha Izazi, parokia ya Isimani. Mwaka 2007 nilihamia Morogoro na kuweka nyumba ya Kitawa.

Mtanzania: Kitu gani kilikuvutia kuja Tanzania.

Padri Riccioni: Nilipenda Tanzania tangu nikiwa kidato cha kwanza baada ya kufuatilia maisha na mfumo wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Nilikuwa nikifuatilia mfumo wa maisha yake na serikali yake kwa kipindi kile, haukuonesha kuwa  yeye ni mtu mwenye kujikweza kuliko  wengine bali alitamani kuishi maisha kama walivyo wengine na si maisha ya kusujudiwa kama mfalme ama kiongozi mkubwa.

Maisha ya baba wa taifa yalinivutia na kunifanya kufikiria kufika Tanzania na kuanza maisha ya utume kwa kujua ni sehemu salama na yenye amani.

Mwalimu Nyerere aliishi maisha ya kitume hata ukiangalia maisha yake hayakufanana na uongozi aliokuwa nao ukilinganisha na wengine.

Mtanzania: Kwanini unapenda kuishi maisha duni na ya kimasikini.

Padri Riccioni: Ni kweli nimechagua kuishi maisha duni licha ya kuwa natoka katika  familia yenye uwezo  mkubwa sana.

Maisha haya ni ambayo mitume wengi waliishi katika mfumo huu.

Najua watu wengi wanashangaa kuniona mimi natembea bila viatu na nguo zangu nikishona kwa sindano ya mkono, lakini maisha haya ndio yenye amani kama ilivyokuwa kwa Yesu na wanafunzi wake.

Mtanzania: Kutokana na maisha uliyochagua ya kulala chini, kutembea pekupeku jamii inakuchuliaje kwa sababu ni vigumu kumuona mzungu akiishi maisha kama  yako hapa nchini.

Padri Riccioni: Kweli wengi hulazimika hata kuacha shughuli zao na kuduwaa wakinitizama nikiwa natembea bila viatu nyakati za jua kali, na hata mara nyingine huwa napenda sana kutumia baiskeri kwa safari zangu za kuzungukia shule zangu, lakini wengi wameshanizoea.

Nimeishi maisha haya kwa zaidi ya miaka 64, sikijui kitanda, wala kiatu na vazi langu ni kama unavyoliona na maisha yanaendelea. Sina muda wa kufikiria mavazi, muda wangu mwingi huwa nautumia kwa kusali na kumuomba Mungu.

Mtanzania: Shule ya Alfa Gems inachukua wanafunzi wa aina gani.

Padri Riccioni: Kwa sasa tuna wanafunzi 5,000 kwa kuwa tumeongeza madarasa mengine katika Shule  ya Sekondari ya Kigurunyembe na Malati.

Shule hii ilianzishwa kwa lengo la kuwapatia malezi na elimu ya sekondari wasichana walioshindwa kupata  elimu kutokana na hali ya kiuchumi katika familia zao.

Shule yetu si ya watoto wa vigogo bali ni ya matabaka ya chini ili kuwawezesha watu wengi kupata elimu na kuchangia ujenzi wa Taifa.

Elimu inayotolewa shuleni hapa ni kwa kudai ada tu iliyopangwa na serikali kwa ajili ya shule binafsi na si zaidi ya hapo.

Shule yetu haina matabaka ya kidini wala kabila lakini wapo watawa wa kanisa katoliki ili kuinua nidhamu na maadili.

Mtanzania: Nini siri ya shule yako kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

Padri Riccioni: Wakati wa usaili huwa tunachagua wanafunzi wenye uwezo mkubwa na walimu ndio wenye uwezo wa kuifikisha shule hapa ilipo.

Walimu wanafundisha kwa kusimamia taaluma na maadili, mara nyingi vijana wanaharibika kutokana na mmonyoko wa maadili kwa walimu wenyewe na wanafunzi.

Shule yetu iko makini sana kusimamia eneo la maadili kwa walimu na wanafunzi.

Lakini lingine ni kujali mafundisho ya dini kwa mujibu wa imani  ya mtu, serikali  imepanga kila wiki  kuwa na vipindi viwili  vya dini shuleni kwa lengo kuwajenga kiimani na maadili wanafunzi.

Mtanzania: Kwa nini wanafunzi wanasoma katika mazingira magumu kuanzia darasani hadi mabwenini.

Padri Riccioni: Ni kweli wanasoma katika mazingira magumu kutokana na darasa moja kuwa na wanafunzi wengi lakini kwa upande wetu tunaangalia kiwango cha elimu tunayotoa kwa wanafunzi wetu.

Tunatoza ada ndogo kuliko shule zingine za binafsi hapa nchini.

Kwa sasa tuna walimu 46 ambao hulipwa mshahara kutokana na ada hiyo ndogo inayotolewa na fedha zingine hutumika kwa ukarabati wa shule.

Mtanzania: Je, ulishawahi kuomba msaada wa kuboresha shule yako.

Padri Riccioni: Mara nyingi huwa nafanya hivyo, tangu mwaka 2009 nimeshajaribu zaidi ya mara 10 lakini mara ya mwisho nilijibiwa kuwa hakuna msaada wa aina hiyo kwa shule binafsi kwani serikali imejipanga kusaidia shule za serikali tu.

Mtanzania: Je, una ushauri gani kwa serikali.

Padri Riccioni: Kwanza kabisa serikali kupitia Wizara ya Elimu inatakiwa kuacha kubadili mitaala kama nguo, kwani kufanya hivyo ni kuwayumbisha wanafunzi na hata walimu, lakini lingine serikali inatakiwa kuacha kupuuzia masomo ya dini na mitihani yake kutotambulika na kutohesabiwa katika ufaulu.

Wachague watoto wenye uwezo wa kiakili pamoja na walimu wanaowajibika katika suala zima la ufundishaji na kusimamia majukumu ipasavyo.

Kutowajibikaji kwa walimu na kutokuwepo kwa uchaguzi mzuri wa wanafunzi wenye uwezo wanaojiunga na shule ndio sababu ya shule nyingi kufanya vibaya.

Pamoja na changamoto nyingi zilizopo lakini bado suala la maadili kwa walimu na wanafunzi halijatiliwa mkazo katika shule nyingi za serikali.

Pia serikali iliangalie suala la wanafunzi kufundishwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwakuwa hata walimu wenyewe wanaofundisha wanafunzi kingereza bado nao hawajui vizuri.

Wengi wao huongea lugha ya Pujini ambayo ni mchanganyiko wa Kingereza na Kiswahili. Tukitumia Kiswahili shuleni taifa litapata wataalamu wengi.

Serikali pia inapaswa kuongeza ushawishi kwa walimu ili kuwafanya wafanye kazi katika mazingira yoyote tofauti na ilivyo sasa ambapo shule nyingi za mjini zimekuwa na walimu wengi kuliko zile za pembezoni kutokana na mazingira mabaya.

Alfa Gems mazingira kama unavyoona ni magumu lakini inatoa elimu bora na walimu wake tumewashawishi kwa kuwalipa stahiki zao vizuri na kwa wakati.

Shule imeendelea kufanya vizuri kwa pindi kirefu ambapo mwaka jana daraja la kwanza ilitoa wanafunzi 41, daraja la pili 96, daraja la tatu 56 na daraja la nne 7 na kuifanya shule kuwa ya 180 kati ya shule 4,795 kitaifa.

Katika matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2015/16 tumefanya vizuri na watu wote mmmeona katika mitandao.

 

MKUU WA SHULE

Mkuu wa shule hiyo, Jonathan Mwachipa, anamzungumzia Padri Riccion na kusema kuwa anapenda kuishi maisha ya kifukara na kwamba mara nyingi hufanya kazi nyakati zote.

“Hata wakati mwingine huamua kushirikiana na mafundi katika ujenzi wa majengo mbalimbali ya shule.

“Ametufanya wafanyakazi wote katika shule hii kuwa familia moja na siku zote amekuwa akisisitiza kuishi maisha ya kiroho kwa mujibu wa imani ya mtu,” anasema Mwachipa.

 

WANAFUNZI

Mwanafunzi Jacqueline Daudi wa kidato cha pili, anasema Padri huyo amekuwa karibu na wanafunzi shuleni hapo kujua kero zinazowakabili katika maisha ya ndani na nje ya shule.

Anasema jambo hilo la kuwa karibu na wanafunzi linajenga wanafunzi kupenda vipindi vyake na mara nyingi hupenda kusisitiza kuhusu suala la hekima, busara na maadili.

Mwanafunzi mwingine Michael Jonathan wa kidato cha tatu, anataja sifa nyingine ya Padri huyo kuwa ni mtu asiyependa uongo, mavazi yasiyo na staa na uchafu.

 

MAJIRANI

Gladnes Urio na Vicent Urio ni mtu na mkewe waliojenga karibu na Shule ya Alfagems.

“Sisi tumezoea kumuita Father Pekupeku, kwa kweli ni mtu mkarimu na ana utani mwingi kwa kila mtu.

“Mara nyingi anapokuta watu husimama na kusalimia na kisha kuendelea na safari zake, ni vigumu sana kusikia analalamikiwa kwa kuwa amekuwa kimbilio kubwa la watu wanaotoka katika familia duni,” anasema Urio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles