24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

PACQUIAO ANAVYOTAMBA KUMZIMISHA MC GREGOR

Manny Pacquiao

 

MARTIN  MAZUGWA NA MITANDAO,

HATIMAYE bondia Manny Pacquiao ameomba pambano dhidi  ya bingwa wa ngumi mchanganyiko, Connor  McGregor, ambaye anakuja juu na kuwa tishio.

Emmanuel Dapidran Pacquiao, bondia mkazi wa Manila, Ufilipino, mwenye  majina mengi kama vile Pac Man, The Destroyer, Manni Pakyyao, The Mexicutioner, Mp na mengine mengi,  lakini wengi  hupenda kumuita Manny  Pacquiao, ni kati ya mabondia bora zaidi hivi sasa duniani kutokana na rekodi zake.

Bondia huyo, ambaye amecheza jumla ya mapambano 67, huku akiwa amepoteza mara sita na kushinda mapambano 38 kwa KO, si wa kubezwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kurusha makonde, huku mkali huyo akiwa ni bondia mwenye spidi zaidi ya kurusha ngumi.

Pac Man (38), mwenye urefu wa futi tano pamoja na uzito wa kilo 144, amekuwa nje ya ulingo tangu Novemba 5, mwaka jana, aliposhinda pambano lake dhidi ya Jesse Vargas, lililofanyika jijini Las Vegas, nchini Marekani.

Mkali huyo amechoshwa na tambo za Mc Gregor, raia wa Ireland, ambaye amekuwa akijisifu kuwa yeye ni bora na hakuna bingwa yeyote anayeweza kumdondosha ulingoni hivi sasa kutokana ubora wake.

Tambo hizo zimekuwa zikiwafanya wakali hao wa mchezo wa masumbwi kumtaka ulingoni mapema mbabe huyo na kumaliza utata baina yao.

Kuonyesha kuwa amedhamiria juu ya jambo hilo, tayari promota wake, Bob Arum, ameongea na waandishi wa habari kuthibitisha taarifa hizo, akisema kuwa, anafahamu kuwa mkali huyo anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya bingwa asiyepigika, Floyd Mayweather, ambaye wamekuwa wakitupiana vijembe mara kwa mara katika mitandao ya kijamii, lakini pia mteja wake anatamani kupanda ulingoni dhidi yake.

Arum anasema kuwa, Pacquiao hatakuwa na pambano jingine mara baada ya kupanda ulingoni dhidi ya bondia anayefanya vizuri hivi sasa raia wa Australia, Jeff Horn, litakalopigwa katika Ukumbi wa Suncorp Stadium Julai 2, hivyo utakuwa wakati sahihi kwa yeye kupanda ulingoni dhidi ya mbabe huyo wa ngumi mchanganyiko.

Promota huyo alisema hayo akihojiwa na kituo cha TMZ kuwa McGregor anapaswa kupanda ulingoni na Pacquiao kama pambano lake dhidi ya bingwa asiyepigika litashindikana.

"Pacquiao anatarajia kuwa na pambano gumu mbele ya bingwa huyo wa Australia, lakini si kigezo cha kushindwa kupanda ulingoni dhidi ya Mc Gregor.

"Mara baada ya pambano la Julai litakalofanyika hapa United States, iwapo kama McGregor bado atakuwa akisubiri kupata mpinzani katika mchezo wa masumbwi, Manny Pacquiao atakuwapo kwa ajili yake," alisema Arum.

"Kwa upande wa McGregor, tayari tumemalizana kila kitu kimekwenda sawa, hivi sasa naanza mazungumzo na kambi ya Mayweather, ambayo pia ina hati miliki yake," alisema bosi wa UFC, Dana White, alipokuwa akifanya mahojiano na kituo cha TNT.

McGregor, bingwa asiyeisha vituko, tayari amethibitisha kusaini mkataba wa kucheza mchezo wa masumbwi na kuweka rekodi ya aina yake katika mchezo wa ngumi mchanganyiko.

"Ni jambo la heshima kusaini na kuweka rekodi ya aina hii, hakika ni furaha kubwa kufanya hivi nikiwa karibu na mshauri wangu, Zuffa LLC,” alisema McGregor.

Iwapo mipango itakwenda kama ilivyopangwa, huenda pambano hilo likapigwa Septemba 16, mwaka huu, ikiwa ni tarehe iliyopendekezwa na upande wa Pac Man ambao ndio walioomba pambano hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles