24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

PACHA WALIOUNGANA WAFARIKI DUNIA DAR

VERONICA ROMWALD Na ABDALLAH NG’ANZI (Tudarco)

-DAR ES SALAAM

PACHA wa kike waliozaliwa wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo, waliokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, wamefariki dunia.

Taarifa ya awali ya madaktari inaeleza pacha hao walizaliwa Julai 21, mwaka huu huko mkoani Morogoro katika Kituo cha Afya cha Berege, kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Julai 24, mwaka huu, pacha hao walihamishiwa Muhimbili kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu zaidi ya kibingwa.

Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Neema Mwangomo, alithibitisha kufariki dunia kwa watoto hao.

“Watoto hao tuliwapokea kutoka Hospitali ya Rufaa Morogoro Julai 24, mwaka huu. Walilazwa katika wodi ya wazazi, lakini baadae madaktari walishauri wahamishiwe katika wodi ya uangalizi maalumu (ICU) kwa sababu hali zao hazikuwa nzuri,” alisema.

Alisema katika wodi ya ICU ambako walihamishiwa, waliendelea kupatiwa uangalizi wa karibu kila wakati na kwamba hali zao ziliimarika.

“Lakini kwa bahati mbaya juzi (Agosti 14, mwaka huu) hali zao zilibadilika ghafla, madaktari walijitahidi kuwasaidia, waliwaongezea hewa ya oksijeni, lakini hata hivyo siku iliyofuata walifariki dunia,” alisema.

Alisema mama wa watoto hao, Rebeka Muya, bado yupo hospitalini hapo akiendelea kupatiwa huduma.

MTANZANIA lilipotaka kujua kama Muhimbili itawatenganisha watoto hao, Daktari Bingwa wa Upasuaji Watoto, Zaitun Bokhary ambaye alikuwa akisimamia matibabu yao hospitalini hapo, alisema familia ndiyo itakayotoa uamuzi iwapo watenganishwe au la.

Hivi karibuni, daktari huyo alisema uchunguzi wa awali ambao watoto hao walifanyiwa, ulibaini kwamba walikuwa wameungana katika sehemu ya kifua na tumbo, ingawa kila mmoja alikuwa ana viungo vyake vya ndani na mfumo wake wa damu.

Alisema pamoja na hayo, ilionekana katika baadhi ya viungo ikiwamo moyo na ini, walikuwa wakishirikiana.

“Kwa mfano kwenye moyo imeonekana wanashirikiana baadhi ya chemba (vyumba), lakini hilo halizuii kuwatenganisha… inawezekana, Muhimbili tunao uwezo wa kufanya upasuaji huo, lakini huwa unashirikisha wataalamu wengi, zaidi ya 20.

“Nchi ambazo zinafanya upasuaji wa aina hii kwa ufanisi duniani ni India na Saudi Arabia, kuwafanyia upasuaji lazima wafikishe miezi sita tangu kuzaliwa ili miili yao iweze kuhimili dawa za usingizi na upasuaji wenyewe ambao huchukua hadi saa 20 kuweza kumalizika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles