31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

PAC yalia wafanyabiashara kukimbia bandari ya Dar es Salaam

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesikitishwa na kitendo cha wafanyabiashara wakubwa kuihama bandari ya Tanzania na kupitishia mizigo yao kwenye bandari za nchi nyingine.

Hayo yalielezwa    jijini hapa jana  na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka   kamati hiyo ilipokutana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Kaboyoka alisema ipo haja kwa sheria kufanyiwa maboresho ya haraka maana tahadhari isipochukuliwa mapema bandari hiyo itakufa kwa kipindi cha muda mfupi.

Alisema ili kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi, watapeleka ripoti ya changamoto zilizopo ndani ya TPA ikiwa ni pamoja na kupitiwa kanuni na vifungu mbalimbali   maboresho ya haraka yafanyike na wafanyabaishara warudi kama ilivyokuwa awali.

“Kamati haikufurahishwa na wafanyabiashara wakubwa kuhama, kuna changamoto ambazo zimefungamana na sheria zilizopitishwa na bunge hivyo inabidi ziangaliwe upya na kuboreshwa,”alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Profesa Ignas Rubaratuka, alisema katika kipindi cha mwaka 2017/18 mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 734 hadi Sh bilioni 838.

Alisema kwa sasa bodi imepata kibali cha muundo mpya ambao unapaswa kutekelezwa kuanzia Januari mwakani.

Profesa Rubaratuka alisema kukamilika kwake kutaongeza kasi ya kutekeleza miradi ya Tehama.

Akizungumzia suala la mapato, alisema  yameongezeka ambako mwaka 2015/16 yalikuwa Sh bilioni 703, 2016/17 Sh bilioni 743 huku 2017/18 ikikusanya Sh bilioni 838.

Pia alisema mwaka 2015/16 zilishuka shehena tani milioni 15, 2016/17 tani milioni 14.7 huku mwaka 2017/18 tani milioni 16.2 jambo ambalo linaonyesha ongezeko kubwa.

Alisema  gawio linalotolewa kwa Serikali limeongezeka kutoka Sh bilioni 92 mwaka 2015/16, Sh bilioni 106 kwa mwaka 2016/17 na kufikia  Sh bilioni 254 kwa mwaka 2017/18.

Vilevile, alisema TPA kwa sasa inatekeleza miradi mbalimbali ikiwamo upanuzi wa bandari za Mtwara na Tanga na ujenzi wa gati.

Alieleza  changamoto zilizopo kwa sasa kuwa ni pamoja rasilimali watu ambako awali walikuwa 3,300 lakini sasa wapo 2,650 na kwamba upungufu huo umetokana na 749 kusimamishwa kazi kutokana na tatizo la vyeti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles