PABLO ESCOBAR ALIVYOANZA UHALIFU HADI KUWA TAJIRI WA KUTISHA – 2

0
684

 

 

NA LUQMAN MALOTO,

Vesco pia anahitaji nafasi yake lakini kwa hapa, uhusika wake ni jinsi ambavyo Pablo aliwatumia Carlos na Vesco kununua Kisiwa cha Norman’s Cay kilichopo Bahamas ili kurahisisha biashara ya cocaine.

Baada ya Pablo na Carlos kukibaini Kisiwa cha Norman’s Cay kama kituo kizuri cha kufanikisha kusafirisha cocaine, waliona pia kwamba endapo kisiwa hicho kingekuwa na wakazi wengine, maisha yangeweza kuwa magumu.

Hivyo basi, uamuzi ukawa kununua kisiwa chote. Carlos na Vesco ndiyo waliokinunua kisha wao wakawa wanaishi Norman’s Cay. Pablo kazi yake ikawa kutuma mzigo kwenda Norman’s Cay kwa meli na wakati mwingine kwa ndege.

Unaweza kuongeza kuwa katika mali alizomiliki Pablo wakati wa uhai wake, ongeza pia na meli kadhaa na maboti makubwa ya mwendokasi ambayo yalibeba cocaine kutoka Norman’s Cay kwenda maeneo mengine yaliyokusudiwa.

Kisiwa cha Norman’s Cay kilitengenezwa vizuri na kisasa kabisa. Carlos na Vesco waliuziwa ardhi ya Norman’s Cay na mamlaka ya Bahamas kama wawekezaji. Na ili wasishtukiwe, walijenga hoteli za za kitalii zenye hadhi kubwa, viwanja vya ndege, bandari na nyumba za makazi.

Kisiwa cha Norman’s Cay kikanawiri kwa ndege zilizoruka na kutua. Maboti yaliyong’oa na kutia nanga hali kadhalika meli. Wakazi wengine wa Bahamas walikitamani Kisiwa cha Norman’s Cay. Fedha za Pablo zilikibadilisha kabisa kisiwa hicho na kuwa na mvuto wa aina yake.

Mambo yaliyofanyika Norman’s Cay si hayo tu, kwani Carlos na Vesco kwa mwongozo wa Pablo, walitengeneza ghala kubwa lenye ubaridi mkubwa kwa ajili ya kuhifadhia cocaine ili ikae kwa muda mrefu ikiwa na ubora wake.

Ndani ya ghala hilo, hali ya hewa yake ilikuwa sawa na friji kutokana na ubaridi wake. Kila jambo lililofanyika ndani ya Norman’s Cay lilikuwa na hadhi kubwa kutokana na fedha za cocaine kutoka kwa Pablo, akiwatumia washirika wake Carlos na Vesco.

Kuanzia mwaka 1978 mpaka 1982, Norman’s Cay ndiyo ilikuwa njia kuu ya kusafirisha cocaine iliyotumiwa na Medellin katika eneo lote la Caribbean na kusambaza maeneo mengine lakini kwa wingi zaidi waliingiza Marekani.

Norman’s Cay ikageuka maficho ya Carlos na Vesco baada ya habari za wao kutafutwa na Marekani kuvuja. Vilevile Norman’s Cay ikawa sehemu salama kwa Carlos na Vesco kuhusika na biashara ya cocaine chini ya Pablo pasipo kugundulika.

Mahitaji yalipokuwa makubwa, usafirishaji ulitakiwa wa haraka pia. Kutokana na hali hiyo, maboti na meli zilitumika kufikisha mizigo maeneo ya karibu au kurahisisha kufikisha kwenye maeneo ambayo helkopta zingebeba.

Mtindo rasmi ambao ulitumika zaidi ni kusafirisha cocaine kutoka Colombia kwa kutumia ndege kubwa aina ya jet, baada ya hapo mzigo ulipokelewa Norman’s Cay na vijana wa Medellin chini ya usimamizi wa Carlos na Vesco.

Baada ya mzigo kupakuliwa kwenye jet, uliwekwa kwenye ghala na baadaye kupakiwa kwenye ndege ndogo-ndogo hadi kwenye maeneo mengine yaliyotakiwa kufikishwa, hasa mpaka wa Marekani. Cocaine ikishafikishwa mpakani na ndege ndogo ilipakuliwa na kuingizwa Marekani kwa usafiri wa barabara.

Cocaine ambayo ilipitia Norman’s Cay, ilipoingizwa Marekani, vituo vyake vikuu vilikuwa kwenye majimbo ya Georgia, Florida na Carolina zote mbili, kwa maana ya Kusini na Kaskazini. Baada ya hapo mzigo ulienea Marekani yote.

PABLO NA SIASA

Pablo alikuwa na kila kitu. Fedha zilimfanya dunia aione nyepesi katikati ya uhusika wake wa biashara haramu na mauaji. Hakuishia hapo, aliingia kwenye siasa na kupata uongozi ndani ya Serikali ya Colombia.

Wanasiasa wengi walijipendekeza kwa Pablo kwa sababu ya fedha zake. Kiongozi kuwa karibu na Pablo ilimaanisha kuwa tajiri, maana alikuwa haangalii fedha anazotoa, zilikuwa nyingi mno.

Kutokana na ushawishi wa wanasiasa, vilevile jinsi ambavyo wananchi walivyompenda kwa sababu walimuona mtu mwema mwenye kutoa misaada mingi kwa watu, walimshawishi agombee uongozi.

Mwaka 1982, Pablo alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Colombia kupitia chama cha Liberal Alternative. Nafasi hiyo, ilimpa Pablo mamlaka katika nchi kusimamia ujenzi wa nyumba, viwanja vya mpira wa miguu eneo lote la Mashariki ya Colombia.

Wajibu wake huo aliutekeleza vizuri mno, kwani mahala ambako ilionekana kuna ugumu kutokana na uhaba wa fedha kwa nchi, Pablo alijitolea za kwake na kufanikisha kila malengo na mipango.

Mafanikio hayo ndiyo yaliwafanya watu wampende zaidi Pablo, hawakuambiwa kitu. Alionekana ni kiongozi bora na wapo ambao walipiga kelele kwamba ndiye hasa alifaa kuwa Rais wa Colombia katika zama zake.

Wakati watu wakiwa hawaambiwi kitu kwa Pablo, mauaji nchini Colombia yalishamiri. Umoja wa Mataifa uliitangaza Colombia kuwa kitovu cha mauaji duniani. Marekani ikamtangaza Pablo kuwa ndiye mhusika wa mauaji hayo kutokana na vitendo vyake vya kikatili katika biashara ya cocaine.

Tangazo hilo la Marekani kuwa Pablo ndiye alikuwa kitovu cha mauaji ya Colombia, Liliwaudhi wananchi wengi wa Colombia. Waliona wanamsingizia kwa chuki zao binafsi, kwani kwa macho na ufahamu wao, hakuna binadamu mwema kupata kumshuhudia kama Pablo.

Itaendelea wiki ijayo…

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here