Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Kampuni Oval Technologies Limited, imetoa rai kwa kampuni changa (Startups) kushiriki kwenye maonyesho ya teknolojia ili kujifunza na kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali.
Hayo ameyasema Novemba 9,2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Ally Salum katika maonyesho ya teknolojia za kifedha yaliyofanyika kweny Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius nyerere (JNICC ).
Salum ambaye yao kampuni yao inajihusisha na utengenezaji wa mifumo ya kompyuta, amesema nchi imepiga hatua kubwa katika ukuaji wa kidigitali ni vyema kampuni za kiteknolojia kushirikiana ili kuhakikisha lengo la serikali linatimia.
“Sisi ni mara yetu ya kwanza kushiriki maonyesho tangu kuanzishwa kwa kampuni yetu mwaka 2018 lakini tumepata fursa ya kujifunza kwa wengine, hivyo tutaendelea kushiriki kila mwaka,” amesema Salum.
Ameongeza kuwa kupitia maonyesho hayo wameweza kubadilishana mawazo na kampuni nyingi na wametanua wigo wa biashara yao na kupata wadau kutoka mataifa mbalimbali.
Akizungumzia kampuni amesema kupitia mifumo wanayoitengeneza wameweza kuwa na mfumo unaoweza kusimamia vikundi vya kijasiliamali na miradi ya kikundi na wafanyabiashara wote.
Amesema wana mfumo unaoweza kusimamia makampuni katika uendeshaji wa idara zake lakini pia usalama mahala pa kazi.
“Mfumo huu ambao tunao unasaidia kusimamia miradi unaweza kujua mradi unaanza lini na unaisha lini na fedha kiasi gani, rasilimali watu, fedha na mali zote mfumo unasaidia kila kitu,”amesema.
Sambamba na hayo pia wametengeneza mfumo kwa ajili ya wafanyabiashara unaofahamika kama ‘smart mauzo’ ambao unawasaidia kufuatilia mwenendo wa biashara zao.