Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA) umesema magonjwa yanayotokea sehemu za kazi yamepungua kutoka 140 mwaka 2019/2020 hadi 109 mwaka 2021/2022.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Machi 4, 2023 na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli zake.
Mwenda amesema kupungua kwa visa hivyo kumechangiwa na kuimarika kwa mifumo ya usimamizi ya OSHA.
Mwenda amesema ajali na magonjwa yanayotokea sehemu za kazi mara nyingi huripotiwa katika maeneo ya kazi za ujenzi na viwanda.
Aidha, Mwenda amesema ajali zinazotokea sehemu za kazi zimepungua kutoka ajali 2,138 hadi ajali 1,855 zilizotokea katika kipindi cha miaka miwili kabla ya uongozi wa RaisDk. Samia Suluhu Hassan.
“Takwimu hizi zinaonesha kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya ambapo imesababisha ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kupungua”amesema Mwenda.
Pia amesema katika kipindi cha miaka miwili wamesajili maeneo ya kazi 1,1953 ikiwa ni ongezeko kutoka sajili 4,336 sawa na asilimia 276 huku kaguzi zilizofanywa zikiongezeka kutoka 104,203 hadi 322,241 kipindi cha 2019/2020.
Aidha, wakala huo umetoa mafunzo kwa wafanyakazi 43,318, na kufanya kufika lengo la kutoa mafunzo kwa wafanyakazi 32,670.
“Pia tunatoa mafunzo baada ya kufanya ukaguzi na kugundua kuna hitilafu kwenye mifumo ya usalama mahali pa kazi na katika hilo tumetoa hati ya marekebisho ya mifumo 1,588 katika kipindi cha miaka miwili 1,588,”amesema Mwenda.