33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

OSHA: Mazingira salama ya kazi ni haki ya msingi ya mfanyakazi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waajiri kote nchini wametakiwa kuhakikisha uwepo wa mazingira salama ya kufanyia kazi ili kuendana na sheria za ndani na kimataifa.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa OSHA, Netiwe Mhando, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Majadiliano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa sekta ya utalii kilichofanyika jijini Arusha Januri 6, 2023.

Wafanyabiashara wa Mkoa wa Njombe wakifuatilia Mkutano wa Saba wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Njombe uliofanyika  katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe ambapo OSHA ilikuwa ni miongoni mwa Taasisi zilizoshiriki katika mkutano huo.

OSHA ilikuwa miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizoalikwa katika kikao hicho kwa ajili kusikiliza na kutolea ufafanuzi changamoto za wadau zinazohusu utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake.

Mkurugenzi huyo amesema katika Mkutano wa 110 wa Kimataifa wa Masuala ya Kazi uliofanyika mwezi Juni, 2022 Geneva Uswisi, suala la afya na mazingira salama ya kazi liliainishwa kuwa miongoni mwa haki za msingi za mfanyakazi mahali pa kazi na hivyo kuzilazimu nchi zote ambazo ni wanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Tanzania ikiwemo, kutekeleza Mkataba wa Kimataifa Namba 155 unaozitaka Serikali katika nchi wanachama kuwa na utaratibu na sera ya kitaifa ya usimamizi wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa OSHA, Netiwe Mhando akiwasilisha mada inayohusu umuhimu wa kutekeleza sheria na miongozo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wadau wa sekta ya utalii wakati wa kikao cha wadau hao kilichofanyika jijini Arusha kikishirikisha wadau na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara, Dk.Godwill Wanga, (hawapo pichani).

Aidha, Mhando amesema Taasisi ya OSHA imejipanga kushughulikia changamoto zilizoainishwa na wadau wa sekta ya utalii na sekta nyingine likiwemo suala la ratiba za ukaguzi kutojulikana na hivyo kuathiri utoaji huduma ambapo amesema wadau hao watakaguliwa kupitia mpango wa ukaguzi wa kisekta.

“Msimu ujao wa ukaguzi wadau wa utalii watakaguliwa kwa wakati mmoja katika kipindi ambacho hakina watalii wengi na hivyo kuwawezesha kukidhi viwango vya usalama bila kuathiri biashara zao,” amesema Mhando.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi wa OSHA, Dk. Jerome Materu, amesema Taasisi ya OSHA inafanya jitihada kubwa katika kutekeleza andiko la serikali la uboreshaji wa mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini (Blue Print) ambapo miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na OSHA ni pamoja na kuondoa tozo zaidi ya 11 zilizoonekana kuwa kero kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini.

“Baada ya kuondoa tozo, sasa tunakwenda kwa wadau kupitia majukwaa mbali mbali kama haya kwa ajili ya kufahamu changamoto zinazowakabili katika kutekeleza taratibu za usalama na afya mahali pa kazi ili tuweze kuzitatua na hivyo kuendelea kuhamasisha uzingatiaji wa masuala ya usalama na afya kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu,” alieleza Dk. Materu.

Kaimu Mkurugenzi wa Usalama na Afya, Dk. Jerome Materu (wakwanza kulia mstari wa pili), Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa OSHA, Netiwe Mhando (watatu kulia mstari wa pili) pamoja na Mkaguzi wa Afya wa OSHA, Dk. Kihama Kilele (wapili kulia mstari wa pili) wakiwa katika Mkutano wa Saba wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Njombe.

Aidha, Dk. Materu amesema katika kipindi hiki ambacho Tanzania imekuwa ikipokea watalii wengi hususan baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kufanya uhamasishaji kupitia filamu ya The Royal Tour, kuna umuhimu wa wadau wa sekta husika kuwekeza katika masuala ya Usalama na Afya ili kukidhi vigezo mbali mbali vya Kimataifa na hivyo kuendelea kuwavutia wageni wengi zaidi kuja nchini.

Kikao hicho cha wadau wa sekta ya utalii kilichofanyika jijini Arusha Januari 6, mwaka huu kilitanguliwa na Mkutano wa Saba wa Baraza la Wafanyabiashara wa Mkoa wa Njombe uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmshauri ya Mji wa Njombe Januari 5, mwaka huu ambapo OSHA ilialikwa kutoa mada pamoja na kusikiliza na kutoa ufafanuzi wa changamoto mbali mbali zinazohusu Usalama na Afya mahali pa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles