30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

OSHA, Idara ya Usalama na Afya Zanzibar kushirikiana kulinda nguvu kazi nchini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi,Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Dk. Islam Seif Salimu ameipongeza OSHA kwa hatua kubwa inazoendelea kufanya za kulinda nguvu kazi kwa kuhakikisha inaweka mifumo Madhubuti ya usalama na afya katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji – Zanzibar, Dk. Islam Seif Salim akizungumza na viongozi wa Menejimeniti ya OSHA Pamoja na baadhi ya Watendaji waandamizi kutoka Idara ya Usalama na Afya Zanzibar wa Idara ya Usalama na afya mahali pa kazi alioambatana nao katika ziara ya kutembelea Ofisi za OSHA kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

Dk. Seif amesema hayo jijini Dar  es salaam baada ya Watendaji waandamizi kutoka Idara ya Usalama na Afya Zanzibar kufanya Ziara Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali Kazi (OSHA) kwa lengo la kujifunza namna taasisi hio inavyosimamia sheria ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi.

“Kimsingi OSHA imepiga hatua kubwa sana katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo niwapongeze sana kwa kuweka mifumo madhubuti katika usimamizi wa masuala mbalimbali ya usalama na afya kazini hivyo tumeona kuna haja kubwa ya kuja katika taasisi hii kujifunza na kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ikiwemo kutengeneza mkakati wa pamoja wa kuhakikisha maeneo yetu ya kazi yanakuwa salama,” alisema Dk. Salim.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema kuwa taasisi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano na Idara ya Usalama na Afya ya Zanzibar ili kujenga ustawi wa wafanyakazi wote nchini.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akitoa neno la ukaribisho kwa katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji – Zanzibar, Dk. Islam Seif Salim pamoja na Watendaji waandamizi kutoka Idara ya Usalama na Afya Zanzibar  Idara ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi alioambatana nao katika ziara ya kutembelea Ofisi za OSHA Dar es Salaam.

“Tumekuwa na ushirikiano mzuri sana na wenzetu wa Wazanzibar katika mambo mbalimbali kiwemo usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, ziara hii imejikita zaidi katika kujifunza namna tulivyofanikiwa kutoka katika kitengo ndani ya idara ya kazi mpaka kujitengemea kama wakala na tunaamini kuwa itawapa chachu ya kufanya mapinduzi juu ya uboreshaji wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi,” alisema Mtendaji Mkuu,  Khadija Mwenda nakuongeza kuwa:

“Tumeshuhudia Zanzibar ikikua kiuchumi kwa haraka sana na shughuli nyingi za kiuchumi zinapofanyika zinakuja na vihatarishi ambavyo vinahitaji mbinu mbadala ya kukabiliana navyo na ndio maana wamekuja kujifunza ni namna gani sisi tumeweza kufanya usimamizi lakini zaidi tutakuwa na ushirikiano mzuri katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ili kujenga ustawi wa wafanyakazi wote nchini” 

Meneja wa Usalama wa OSHA, Mhandisi Robert Mashinji (kulia) akiwasilisha mada mbele ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Dk. Islam Seif Salim (hayupo pichani) pamoja na Watumishi wengine wa OSHA na Idara ya Usalama na Afya Zanzibar.

Aidha, Mkurugenzi wa Idara ya OSHA Zanzibar, Dk. Ali Said Nyanga amesema kupitia ziara hii itawasaidia kutatua changamoto mbalimbali walizokuwa wakikumbana nazo wakati wakitoa huduma vilevile itawasaidia kulinda nguvu kazi kwa kuhakikisha mazingira yote ya kazi yanakuwa salama.

“Tumekuwa tukikumbana na changamoto mbalimbali katika utoaji huduma na  changamoto hizo zimepatiwa majibu mahali hapa pia tumeshuhudia ongezeko kubwa sana la uwekezaji nchini ambao utahitaji sana huduma zetu hivyo nilazima tuhakikishe nguvu kazi hizi zinalindwa ipasavyo iliziweze kuzalisha mara dufu” alisema Mkurungezi wa Idara ya Usalama na Afya kazini, Dk. Nyanga.

Idara ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini Zanzibar ni idara iliyo chini ya Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji yenye jukumu la Kusiamia masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi Tanzania Visiwani (Zanzibar).

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji – Zanzibar, Dk. Islam Seif Salim (aliyekaa mbele), Watendaji waandamizi kutoka Idara ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Zanzibar pamoja na Viongozi wa Menejimenti ya OSHA wakibadilishana uzoefu juu ya masuala mbalimbali ikiwemo usimamizi wa usalama na afya katika maeneo ya kazi.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles