27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

OSCAR: NAONDOKA LAKINI HAPA NI NYUMBANI

Oscar dos Santos
Oscar dos Santos

LONDON, ENGLAND

BAADA ya klabu ya Chelsea kuthibitisha kwamba nyota wao, Oscar dos Santos, anatarajia kujiunga na klabu ya Shanghai SIPG wakati wa uhamisho wa Januari, nyota huyo amewaaga mashabiki na kudai kwamba bado Chelsea itakuwa kama nyumbani kwake.

Mchezaji huyo tayari amefikia makubaliano ya kujiunga na klabu hiyo kwa kitita cha pauni milioni 52 sawa na bilioni 136, huku akitarajia kuchukua kitita cha pauni 400,000 sawa na bilioni 1 kwa wiki.

Hiyo ni historia mpya kwa mchezaji huyo kuja kuwa wa kwanza katika soka kulipwa fedha nyingi duniani.

Mchezaji huyo alikuwa hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha kocha Antonio Conte katika uwanja wa Stamford Bridge, hadi sasa amecheza jumla ya michezo 11 ya Ligi Kuu msimu huu, pia hajapata nafasi ya kuanza katika kikosi hicho tangu katikati ya Septemba katika mchezo ambao Chelsea ilipokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Liverpool.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, mchezaji huyo amewashukuru wachezaji wenzake, viongozi pamoja na mashabiki wa timu hiyo kwa ushirikiano waliouonesha.

“Napenda kutumia nafasi hii kumshukuru bosi wa timu hii, waajiri ambao wamenifanya niwe hapa kwa sasa pamoja na mashabiki wote wa klabu hii, nimekuwa na furaha kuwa mmoja wa wachezaji wa klabu hii kubwa duniani.

“Nimekuwa miongoni mwa wachezaji ambao wameweza kuipa mataji klabu hii kama vile Europa Ligi, Kombe la Ligi pamoja na ubingwa wa Ligi Kuu nchini England.

“Kutokana na hali hiyo naweza kusema kwamba, Chelsea ni sehemu ya maisha yangu, japokuwa naondoka ndani ya klabu hii lakini bado mimi ni sehemu ya klabu hii,” aliandika Oscar.

Klabu ya Chelsea iliandika kwenye mtandao wao kwamba, klabu hiyo na matajiri wa nchini China, klabu ya Shanghai SIPG, zimekubaliana uhamisho wa kudumu wa mchezaji huyo.

“Tumefikia makubaliano na klabu ya Shanghai SIPG kuwauzia kiungo wetu Oscar, kwa pamoja tunamtakia maisha mema katika makazi yake mapya kwa maisha yake ya baadaye,” waliandika Chelsea.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, Hulk, aliweka rekodi ya usajili na kujiunga na klabu hiyo ya SIPG, Juni mwaka huu kwa kitita cha pauni milioni 47, sawa na bilioni 122, huku kwa wiki akichukua pauni 320,000, sawa na milioni 837 kwa wiki, akitokea klabu ya Zenit St Petersburg.

Kutokana na uhamisho huo, Oscar atakuwa anashika nafasi ya kwanza duniani kulipwa fedha nyingi akifuatiwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambao wanachukua pauni 365,000 kwa wiki sawa na milioni 955, huku kwa mwaka wakichukua pauni milioni 19 sawa na bilioni 49, wakati huo Oscar akichukua pauni milioni 20 kwa mwaka sawa na bilioni 52.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles