23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ORODHA YA MADHARA YA TUMBAKU HII HAPA

 

Na SARAH MOSES–DODOMA

IMEELEZWA kuwa mtu mmoja kati ya watatu hufariki dunia kutokana na saratani inayosababishwa na matumizi ya tumbaku.

Hayo yalisemwa na Rais wa chama cha wanafunzi wafamasia Tanzania (TAPSA), Erick Venant, wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege jijini hapa.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali inatakiwa kuimarisha kanuni za kukataza matumizi ya tumbaku ili kulinda afya za wananchi.

Pia alibainisha kuwa mtumiaji mmoja wa tumbaku kati ya nane hufariki dunia kutokana na ugonjwa wa moyo.

“Bado kuna tishio kwa kuwa watu wengi hawafahamu uhusiano kati ya kuvuta tumbaku na magonjwa ya moyo,” alisema Venant.

Alisema licha ya tumbaku kuwa zao la biashara linalochochea uchumi nchini, bado watumiaji wake wana uwezekano mkubwa wa kupata vidonda vya tumbo.

“Wanawake wajawazito wanaovuta sigara wanajiweka katika uwezekano mkubwa zaidi kujifungua mtoto njiti au mwenye uzito mdogo,” alisema Venant.

Mfamasia huyo alibainisha kuwa uvutaji wa sigara katika maeneo yasiyo rasmi hususani majumbani kunaweza kuwaathiri wanafamilia na kusababisha kutumia fedha nyingi katika matibabu.

Akieleza sababu ya kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya tumbaku kwa wanafunzi wa sekondari, alisema wanafunzi hao ni mabalozi wazuri katika kuufikisha ujumbe kwa jamii na kwamba wamefanya hivyo ili kuwachochea kujiepusha na matumizi ya tumbaku.

Naye mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Furaha Kalinga, alisema wanafunzi wa umri wa kati ya miaka 13 na 15 wapo hatarini kutokana na kujaribu kujiingiza katika matumizi hayo.

“Kundi hili lipo hatarini zaidi kwani nimekuwa nikishuhudia baadhi ya wanafunzi wa kiume wakiiga kutumia sigara ilihali kila siku tunaelimishwa kuwa matumizi ya sigara ni hatari kwa afya,” alisema Furaha.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 17.9 hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles