25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

OPERESHENI YA MAKONDA: DAWA ZA KULEVYA SASA KAA LA MOTO

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

HAKUNA msalie mtume. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya agizo la Rais Dk. John Magufuli kwa vyombo vya dola la kuvitaka kukamata kila anayehusika na biashara ya dawa za kulevya, hata kama ni mkewe, Janeth.

Rais Magufuli, alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana, wakati wa kumwapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo.

Alisema vita ya dawa za kulevya si ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pekee, bali ni ya kila mtu kwani dawa hizo zinaangamiza nguvu kazi ya taifa.

Wiki iliyopita, Makonda alitaja wasanii maarufu, akiwamo Wema Sepetu na askari polisi 12  wanaodaiwa kujihusisha na biashara hiyo, hali iliyofanya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu, kuwasimamisha kazi askari hao, huku wasanii waliotajwa wakiendelea kusota rumande.

 Akizungumza jana, Rais Magufuli alimpongeza IGP Mangu kwa hatua yake ya kuwasimamisha kazi askari hao.

 “Nakupongeza sana IGP kwa hatua ulizochukua kwa kuwasimamisha kazi baadhi ya watendaji wako ili uchunguzi ufanyike na nataka kukuhakikishia  umefanya vizuri na umetoa heshima nzuri kwa Jeshi la Polisi.

“Tembea kifua mbele katika vita hii ya madawa ya kulevya, hakuna cha mtu aliye maarufu, hakuna mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri au mtoto wa fulani ambaye akijihusisha aachwe, hata  angekuwa mke wangu hapa Janeth, akijihusisha shika,” alisema Rais Magufuli.

Alisema madhara ya dawa za kulevya yamefikia mahali pabaya.

“Haiwezekani yawe yanauzwa kama njugu. Siyo siri, sote tulio hapa tunajua madawa ya kulevya yanamaliza nguvu kazi ya Watanzania wengi, hasa vijana, kwahiyo naagiza vyombo vyote, Jeshi la Polisi na wengine wote wanaohusika endeleeni kufanya kazi zenu, hii kazi siyo ya Makonda, ni ya Watanzania wote, shika yeyote peleka mahakamani, hakuna cha umaarufu.

 “Mkishika hawa wote wanaovuta madawa ya kulevya, wataeleza ni nani anayewauzia na aliyewauzia mkimshika, ataeleza anayatoa wapi na yeye huyo mkimshika atawaeleza anayapata wapi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kwa kufanya hivyo, kundi lote la watu wanaojihusisha na biashara hiyo litakuwa limeshughulikiwa.

“Najua mtapata vipingamizi vingi, hata IGP najua ulipigiwa simu, wengine wakawa wanakupa ushauri fulani, nashukuru hukuwasikiliza, ungewasikiliza ningejua na wewe unahusika na leo usingekuwa hapa na hicho cheo, kwa hiyo nakupongeza sana umesimama imara,” alisema.

Alisema dawa za kulevya zinaliangamiza taifa, ni lazima kusimama kidete kupambana na vita hiyo na kumtanguliza Mungu ili kuhakikisha Tanzania Bara na Visiwani biashara hiyo inamalizwa.

“Haiwezi ikawa vijana wanaotegemewa kujenga, wakawa ndiyo walevi wa dawa za kulevya alafu wakubwa fulani wanazunguka wanatamba,” alisema.

Alisema pia kesi zinazohusu dawa za kulevya zimekuwa zikichelewa sana kusikilizwa na kufanyiwa uamuzi, suala alilosema anataka libadilike ili na watuhumiwa wakubwa wa biashara hiyo wafungwe tofauti na sasa ambapo wale wadogo ndio wanaoonekana zaidi.

DK. SHEIN

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, pamoja na kuwapongeza viongozi wakuu wapya wa JWTZ na kumshukuru Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange kwa utumishi wake, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ipo tayari kutoa ushirikiano wowote kwa jeshi, huku akibainisha kuwa ana imani kubwa na chombo hicho.

WAAPISHWA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemwapisha Kamishna Juma Malewa kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza.

Kabla ya kumwapisha, Rais Magufuli alimvalisha cheo kipya cha Kamishna Jenerali.

Kamishna Jenerali Malewa, amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna John Casmir Minja ambaye amestaafu.

Rais Magufuli, pia amemwapisha Balozi Luteni Jenerali mstaafu Paul Meela kuwa balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Balozi Luteni Jenerali mstaafu Meela, anachukua nafasi ya Balozi Anthony Ngereza Cheche ambaye amestaafu.

Balozi mwingine aliyeapishwa jana, ni Samuel Shelukindo anayekuwa balozi wa Tanzania nchini Ufaransa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Begum Taj ambaye amestaafu.

Pia Nyakimura Muhoji, aliapishwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Claudia Mpangala ambaye amestaafu.

Rais Magufuli pia alishuhudia kuapishwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz. Aliapishwa na IGP Mangu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles