OPERESHENI UKUTA ILIVYOITIKISA SERIKALI

0
595
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Na LEONARD MANG’OHA- DAR ES SALAAM

MIEZI 12 ya mwaka 2016, ilikuwa ni ya aina yake hasa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, kutangaza operesheni ya Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) ambayo ilikuwa inakwenda sambamba na maandamano nchi nzima.

Operesheni hiyo ilitangazwa kufanyika Septemba Mosi, ambapo pamoja na mambo mengine ilikuwa iambatane na kufanyika kwa mikutano na maandamano nchi nzima.

Hatua hiyo ilizua taharuki kwa Serikali pamoja na wananchi huku vyombo vya dola likiwemo Jeshi la Polisi likilazimika kuandaa askari wake na magari maalumu yaliyokuwa yakiranda mitaani yameandikwa ‘Vunja Ukuta’.

Mbali na hilo pia askari hao walikuwa wakifanya mazoezi katika miji mbalimbali nchini ikiwa ni ishara ya kujiandaa na wafuasi wa Chadema watakaokuwa wamejitokeza kwa lengo la kufanya maandamano mitaani.

Akitangaza maazimio ya kikao cha Kamati Kuu Julai 27, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe, alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kujenga jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.

“Ni wazi sasa kuwa, kuna tishio kubwa dhidi ya ukuaji wa demokrasia hapa nchini mwetu kutoka kwa viongozi wa serikali hii ya awamu ya tano ambao wanakandamiza demokrasia na madhara yameshaanza kulitafuna taifa letu,” amesema Mbowe.

Alitaja baadhi ya matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini kuwa ni kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kufanya mikutano.

Jingine ni kupiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa matangazo ya Bunge na kudhibiti wabunge wa upinzani bungeni kupitia Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Matokeo mengine ni kuingilia mhimili wa mahakama, kupuuza utawala wa sheria, serikali kupeleka mswada kandamizi wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, serikali za mitaa kunyang’anywa mapato na serikali kuu na uteuzi wa wakurungezi, makatibu tawala wa wilaya bila kuzingatia sheria ya utumishi wa umma.

“Mbali na hayo, serikali pia imetoa maelekezo kupitia mawasiliano yake na mabalozi kuelekeza kuwa, kabala ya mabalozi au maofisa wa ubalozi kukutana na asasi zisizo za kiserikali au vyama vya siasa ni lazima kwanza waombe kibali cha serikali kupitia wizara ya mambo ya nje.

Pamoja na mambo mengine, chama hicho kilisema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini, kiliyodai kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumzia chimbuko la Ukuta, Mbowe alisema umetokana na Rais Magufuli kupiga marufuku safari zote za nje kwa watumishi wa umma, kuamuru Mahakama Kuu iwahukumu wafanyabiashara ambao wana kesi za kodi ili Serikali ishinde.

Mbowe alitaja sababu nyingine kuwa ni Serikali kuendeshwa kwa matamko badala ya Katiba na sheria, Serikali kuwafukuza na kuwadhalilisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na mikutano ya kisiasa kupigwa marufuku.

Polisi waonya

Agosti 23 Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kupitia kwa Kamishina Simon Sirro lilipiga marufuku maandamano hayo na kusema hakuna mtu atakayethubutu kuingia barabarani kutokana na jeshi la polisi kujipanga kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao bila kuingiliwa na kitu chochote.

Baada ya marufuku hiyo ya Polisi ilifuatiwa na viongozi wa kiserikali wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambao wote walipinga operesheni hiyo na kusema kuwa ina nia ovu ya kuleta machafuko nchini.

Kutokana na vuguvugu hilo Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilifanikiwa kumtia mbaroni mfanyabiashara mmoja, Yoram Mbyelllah, mkazi wa Mburahati Dar es Salaam kwa tuhuma za kuuza fulana zenye maneno ya uchocezi.

Mbowe ahojiwa

Katika hatua nyingine Agosti Mosi mwaka huu Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisisitiza kuwa licha ya viongozi wa chama hicho kutishwa msimamo wao kuhusu operesheni Ukuta uko pale pale.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam baada ya kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Lissu alisema msimamo wao uko palepale na hakuna kilichobadilika.

“Wamemuhoji kwa taarifa aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama wa kufanya mkutano nchi nzima. Tatizo jeshi letu wakisikia maandamano, mkutano au mtu anamsema Magufuli basi anatuhumiwa kwa uchochezi.

“Wametumia muda mrefu kumuhoji lakini mwisho wamemwachia kwa dhamana na amewahi ‘Airport’ ili aende kuhudhuria mazishi ya kamanda wetu Senga (Joseph) na watamwita watakapomhitaji tena,” alisema Lissu.

Ukuta waahirishwa
Septemba 30 ikiwa zimebaki mbili kabla ya kufanyika kwa operesheni hiyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza kutofanyika kwa Operesheni Ukuta pasi kutaja tarehe ya kufanyika operesheni hiyo kwa kile alichodai ni kutompa adui nafasi ya kujipanga.

Awali operesheni hio ilikuwa ifanyike Septemba Mosi mwaka huu lakini iliahirishwa kutoa nafasi kwa viongozi wa dini kukutana na kujadiliana na Rais Dk. John Magufuli juu ya mustakabali wa hali ya kisiasa nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here