23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Onyesho la Nyerere kufikia tamati Oktoba 14

FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM

ONYESHO la historia la kumuenzi na kutambua mchango wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere katika kupigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika lililoanza Agosti 17, mwaka huu, linatarajiwa kumalizika Oktoba 14.

Siku hiyo ndiyo kilele cha kumbukumbu ya miaka 20 tangu Mwalimu Nyerere kufariki dunia, Oktoba 1999 jijini London, Uingereza.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Joyce Mkinga, alisema onyesho la  kumuenzi Nyerere linatokana na mchango wake mkubwa aliotoa wakati wa uhai wake.

Alisema mchango wake kwa asilimia kubwa ulisaidia nchi za Afrika kupata ukombozi.

“Tukataka kuonyesha ni jinsi gani Mwalimu Nyerere alitoa mchango wake katika nchi za Afrika wakati wa harakati za ukombozi,” alisema.

Alisema kuanzia Agosti 17, mwaka huu walipokea wageni kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambao ni wake wa marais waliokuja kushiriki mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo.

Wake wa marais watano walifika nchini na kutembelea Makumbusho wakiwa na mwenyeji wao, Janeth Magufuli.

Wake hao ni pamoja na mke wa Rais wa Afrika Kusini, Dk. Tshepo Motsepe, mke wa Rais wa Namibia, Monica Geingos, mke wa Rais wa Comoro, Azali Ambari na mke wa Waziri Mkuu wa Eswatini, Jane Dumile Dmlamini.

Joyce alisema pia wake hao wa marais walikutana na Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa Mwalimu Nyerere.

Alisema katika onyesho hilo, kuna vitu mbalimbali ambavyo Mwalimu Nyerere alivitumia kama cherehani, pasi, redio na picha za matukio mbalimbali ya familia yake.

Pia alisema kulikuwa na pikipiki ya zamani aliyokuwa anatembelea Rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Machel wakati wa harakati za ukombozi wa nchi yake.

Alisema onyesho hilo linawafundisha Watanzania namna Mwalimu Nyerere alivyoishi na kusaidia upatikanaji wa uhuru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles