BAADA ya kimya cha muda mrefu, mwanamitindo wa muda mrefu nchini Zanzibar, Waiz Shelukindo, amesema kwamba wapenzi wa mitindo visiwani humo watarajie shoo kubwa ya mitindo mwanzoni mwa Machi, mwaka huu.
Waiz alisema kwa muda mrefu visiwa hivyo vimekosa maonyesho ya mitindo kutokana na kuelekeza shughuli zao nje ya visiwa hivyo, zilizokuwa na lengo za kutanua mauzo na usambazaji wa mavazi ya Kiafrika kwa nchi za nje.
“Kwa muda mrefu hatukufanya onyesho kubwa visiwani Zanzibar, tulikuwa nje ya nchi kwa takribani miezi mitatu, tulikuwa katika ufunguzi wa duka letu la nguo za Kiafrika katika mji wa Milano, nchini Italia, tulilolipa jina Macs African Clothing Supply.
“Pia tulikuwa tukifanya kazi za waonyesha mavazi wa kimataifa ambao wametupa changamoto mbalimbali ambazo zimesaidia pia kufungua duka kubwa la mavazi ya Kiafrika yanayotoka Zanzibar katika eneola Shangani, kwa ajili ya Watanzania na watu wa kutoka nje watakaokuja kutembelea visiwa vyetu,” alieleza Waiz.
Onyesho hilo linalotarajiwa kufanyika visiwani humo mwezi ujao, litashirikisha wanamitindo kutoka visiwani humo na wengine kutoka maeneo yote ya Tanzania bara.