29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

ONEKANA BAHILI LAKINI UNAJUA UNACHOFANYA – 2

Na ATHUMANI MOHAMED

HAUHITAJI nguvu nyingi katika kusaka mafanikio, bali akili na maarifa. Wala siyo lazima sana uwe na elimu ya Chuo Kikuu ili ikiwezeshe kuwa bingwa wa maisha na mafanikio.

Maisha ni wewe. Namna unavyoishi, unavyotenda na kufikiri huakisi maisha yako yajayo. Kwa lugha nyepesi ni kwamba, wewe ndiye mwenye kupanga aina ya maisha unayotaka.

Hakuna mtu wa kuingia kwenye maisha yako na kuyabadili. Ni vile wewe unavyotaka. Ndiyo kusema kwamba, ikiwa utaamua kuishi kimasikini itakuwa hivyo siku zote za maisha yako.

Lakini siku utakayoamua sasa kubadili fikra zako na kuishi kitajiri, bila shaka kila kitu chako kitabadilika na mara moja utaanza kufanya vitu vya kitajiri ambavyo vitakusogeza kwenye mafanikio makubwa.

Nilisema wiki iliyopita kwamba, kuishi kwa kuangalia watu wengine wanasema nini kuhusu maisha yako ni kujidanganya. Hakuna maisha ya namna hiyo.

Wewe ndiye rubani wa maisha yako. Ndiye unayejua unapoelekea na unapotaka kuelekea. Wewe ndiye mwenye kupanga namna unavyotaka iwe. Hakuna mwingine wa kukupangia. Ni wewe.

Achana na kushindana kuhusu mavazi ya gharama au vyakula vya bei mbaya wakati huna akiba. Angalia kile unachoweza kufanya kwa wakati huo.

UNATUMIA USAFIRI GANI?

Je, unatumia usafiri gani kwa ajili ya mizunguko yako? Kuna mwingine hana gari na kwa sasa hana uwezo wa kununua gari, lakini atalazimisha na yeye aonekane na gari.

Anaweza kununua gari ili ajionyeshe lakini akashindwa kulihudumia ipasavyo. Kununua gari kuna suala la mafuta na matengenezo, je utamudu?

Wapo wengine wapo tayari hata kukodisha magari ili aonekane. Atakodi kwa fedha nyingi, lakini hana uwezo nalo. Kipato anachopata hakimruhusu kabisa kukodisha gari, lakini atalazimisha ili ajionyeshe mbele za watu. Hiyo haipo sahihi.

Mwingine kipato chake ni cha kupanda daladala, lakini atalazimisha apande taxi au Bajaj. Pima kipato chako. Hata kama utaona mchungu na mbaili ni sawa tu, maadamu unajua unachokifanya.

 

NYUMBA UNAYOISHI

Je, nyumba unayoishi inalingana na kipato chako? Mwingine analipwa mshahara wa 400,000 lakini anapanga chumba kimoja mjini cha 100,000. Mtu wa namna hii ni dalili kuwa uwezo wake wa kufikiri haupo sawa.

Kwa hesabu za kawaida, unapaswa kuangalia mshahara wako, kisha gawanya kwa tatu. Robo moja iwe ni akiba, robo moja matumizi na robo nyingine dharura.

Je, maisha yako yanaendana na kanuni hiyo ya kijasiriamali? Siyo sahihi kutumia fedha zote leo kwa matarajio ya kupata nyingine kesho. Hizo si kanuni za mafanikio kabisa.

 

VITU VYA ANASA

Utakuta mwingine anatumia simu ya gharama kubwa. Labda tusema simu ya 700,000 wakati mshahara wake ni mdogo wake.

Yanini kujilinganisha na wengine. Ukichunguza sana, utakuja kugundua kuwa mtu huyo alitakiwa kutumia simu ya 40,000 tu lakini analazimisha kuwa na simu zenye mitandao ya kijamii.

Anasahau kwamba, kuwa na simu za namna hiyo kwanza ni kujiongezea gharama. Maana simu za namna hiyo utatakiwa kuwa na bando la intaneti kila siku.

Je, utaweza kumudu gharama hiyo? Tufanye kwa wastani wa chini wa matumizi ya kawaida ni 1000 kwa siku, bado vifurushi vya muda wa maongezi, ambavyo labda ni 500 kwa siku.

Ukipiga hesabu hapo utagundua mtu anapoteza 45,000 kwa mwezi. Mtu ambaye mshahara wake ni 250,000. Kwanini anafanya hivyo? Kwa sababu fulani naye anatumia simu kama hiyo.

Ni fikra zisizo na mashiko hata kidogo. Angalia mbele, maisha ni wewe. Ukifeli utafeli mwenyewe lakini ukifanikiwa, pia itakuwa ni wewe mwenyewe!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles