Omog: Kitaeleweka tu Simba

Joseph Omog
Joseph Omog
Joseph Omog

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MATOKEO ya sare ya kutokufungana kati ya Wekundu wa Msimbazi, Simba na maafande wa JKT Ruvu, bado yanamkosesha raha Kocha wa Simba Mcameroon, Joseph Omog, ambaye ameeleza wazi kuwa atafurahi kama timu yake itapata ushindi, huku akisisitiza kitaeleweka tu kwa wekundu hao msimu huu.

Sare hiyo huenda ikawahenyesha upya washambuliaji wa timu hiyo, kwani Omog anachokitaka sasa kwa timu yake ni kuwa na matokeo mazuri ambayo yatakiwezesha kikosi hicho kutimiza mipango yake ya kutwaa ubingwa.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Omog alisema nia yao ni kutoka na ushindi katika kila mchezo, kwani sare waliyoipata Jumamosi iliyopita hakuipenda ingawa haijavuruga mipango yake.

“Hatukuwa na jinsi mbele ya wapinzani wetu, kwani JKT Ruvu walijipanga na kuweka ukuta imara, hili linatufundisha kujiweka tayari kukabiliana na timu za aina hii.

“Pia matokeo haya yanatukumbusha kwamba tunatakiwa kufanya kazi kwa nguvu hasa kwa washambuliaji, nitaendelea kukinoa kikosi changu ili kiweze kuwa bora zaidi na tayari kwa mapambano muda wote,” alisema.

Aidha, Omog alisema kuwa anaamini wachezaji wake watakuwa wamemwelewa na watafanya kama anavyotaka, ili kuifanya Simba iwe bora zaidi msimu huu.

Simba inatarajia kucheza dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo unaofuatia Septemba 7.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here