30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

OMOG ASANTE, LAKINI INATOSHA SASA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


NI vigumu lakini haina budi kusema viongozi, wadau na mashabiki wa Simba wanatakiwa kumshukuru kocha wa timu hiyo Mcameroon, Joseph Omog na kumpa mkono wa kwakheri kwa kile alichokifanya ndani ya klabu hiyo.

Omog ameweza kuipa Simba jeuri ya kurejea kwenye michuano ya kimataifa mwakani, baada ya kuwa bingwa wa Kombe la Shirikisho kwa kuifunga timu ya Mbao FC kwenye mchezo wa fainali iliyochezwa wiki mbili zilizopita katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Lakini naamini moja kati ya mabadiliko muhimu katika kikosi cha Simba ni kuachana na kocha wake huyo na kutafuta kocha ambaye atakuwa tiba ya kikosi chao baada ya kuwa kwenye hali mbaya misimu minne iliyopita.

Makosa binafsi ya Omog yaliigharimu sana Simba na yalikaribia kuwaangusha katika fainali ya FA dhidi ya Mbao FC.

 Omog inawezekana alifanikiwa kama kocha wakati alipoisaidia AFC Leopard ya Congo Brazaville kushinda ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2012 na akashinda ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/14 akiwa kocha wa Azam FC, lakini Mcameroon huyo ameonyesha wazi kuwa na udhaifu wa kimbinu, huku suala la ufundi likinipa shaka mara kwa mara.

Zipo sababu nyingi ambazo Simba wanaweza kuzitumia kumwondoa kocha huyo hasa kuhusu upangaji wake mbovu wa kikosi wanapokuwa kwenye mchezo muhimu na kama wakipuuzia  hilo, huenda likawagharimu huko waendako katika anga za kimataifa.

 Simba wanahitaji kocha makini mwenye uwezo wa kuwaongoza wachezaji bila kuyumba kimbinu na uwezo wa kufanya mabadiliko na pia kufahamu aina ya wachezaji alionao, lakini si Omog ambaye kama si bahati Simba ingeendelea kuumia moyoni.

Awali Omog alinufaika sana na mbinu ya kushambulia pembeni, lakini mabadiliko yake ya kiufundi mara kwa mara yamekuwa si sahihi.

Matokeo ya msimu uliopita yalionesha wazi kuwa kikosi cha Omog kisingeweza kufunga mabao mengi kwa sababu alishindwa kutengeneza safu ya kwanza na ile ya pili ya washambuliaji kati ya Ibrahim Ajib, Mrundi, Laudit Mavugo, Muivory Coast, Fedrick Blagnon na Juma Liuzio.

Hivyo, kamati maalumu ya usajili ya Simba ambayo imeundwa hivi karibuni mbali na ile ya Zachalia Hans Pope, inayo jukumu la kuliangalia suala hili kwa jicho la kipekee kwa kuwa kwenye michuano ya kimataifa hakuna wa kumlaumu kama hukujipanga sawasawa.

Licha ya Simba kuwa katika harakati za kutafuta wachezaji watakaoongeza nguvu kwenye michuano ya Kimataifa, wanapaswa kumuondoa Omog na kumpa kazi kocha mwingine mwenye uwezo zaidi yake ili kuungana na Mganda, Jaclson Mayanja.

Sababu kubwa ya Simba kufanya mabadiliko ya Omog inatokana na ushiriki wao kwenye michuano ambayo inahitaji zaidi makocha ambao wana mbinu na ufundi mkubwa wa kuvifanya vikosi vyao kucheza vile watakavyo bila kuathiri matokeo yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles