Ombi la akina Mbowe lakwama

0
1197
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia), akimsikiliza Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msingwa, baada ya kesi yao kuahirishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana.

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wenzake, wamegonga mwamba baada ya mahakama kuamuru waanze kujitetea wao badala ya kuanza mashahidi wao.

Uamuzi huo ulitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.

Washtakiwa katika kesi hiyo waliomba mahakama iwaruhusu waanze kujitetea kwa kuwaleta mashahidi kwanza, wakimalizika ndio wajitetee wenyewe.

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai ombi la upande wa utetezi la kuanza kusikiliza mashahidi kabla ya washtakiwa wenyewe kutoa utetezi halitekelezeki kwa sababu linakiuka sheria ya ushahidi na mwenendo wa mashauri ya jinai inayotoa mwongozo wa kuendesha na kusikiliza mashauri.

Akitoa uamuzi, Hakimu Simba alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama imeona hoja za upande wa utetezi hazina msingi na hawajatoa sababu za kutosha kwanini waanze mashahidi badala ya washtkiwa.

“Mahakama inakubaliana na hoja za Jamhuri, inatupilia mbali maombi yaliyowasilishwa kupitia Wakili Peter Kibatala.

“Ni utaratibu wa kawaida mshtakiwa anapokutwa na kesi ya kujibu anasomewa mashtaka upya na kujulishwa haki zake, anajitetea na baadae kuita mashahidi.

“Sioni tatizo washtakiwa kuanza kujitetea kabla ya mashahidi,”alisema.

Wakili Kibatala alikubaliana na uamuzi huo kisha akaomba wapewe wiki tatu za kujiandaa ili Mbowe aanze kujitetea akifutiwa na washtakiwa wengine.

Pia waliomba wapewe picha za video zilizochukuliwa katika mkutano wa kampeni viwanja vya Buibui Februari 16 mwaka jana na vielelezo vingine.

Wakili Nchimbi alipinga muda uliombwa akidai kwamba Septemba 12 walipokutwa na kesi ya kujibu washtakiwa walitakiwa kuanza kujiandaa kwa utetezi.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja hizo imepanga kutoa uamuzi Oktoba 21 mwaka huu.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka 2017, Mbowe na wenzake wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na  wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka 2017 Bulaya alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huo barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washitakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya Ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara mshitakiwa John Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki alitamka matamshi kwamba “Kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii…wizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano…watu wanapotea…watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome… ” alinukuliwa na kudaiwa kuwa maneno yaliyoelekea kuleta chuki kati ya serikali na watanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here