27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Omar al-Bashir atupwa jela Sudan

KHARTOUM, SUDAN

RAIS aliyepinduliwa madarakani na jeshi nchini hapa, Omar al-Bashir, ametupwa gerezani baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia jana.

Bashir aling’olewa madarakani wiki iliyopita katika mapinduzi ya kijeshi baada ya kuiongoza Sudan kwa miaka 30.

Vyanzo vya habari kutoka familia ya Bashir, vimethibitisha kuwa kiongozi huyo mwenye miaka 75 amekamatwa na kupelekwa jela.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Bashir anashikiliwa kwenye chumba cha pekee cha gereza lenye ulinzi mkali la Kobar mjini Khartoum. Awali kiongozi huyo alikuwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi nyumbani kwake tangu alipopinduliwa wiki iliyopita.

Sudan kwa sasa ipo chini ya uongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi linaloongozwa na Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan.

Katika hotuba kwenye televisheni siku ya Jumamosi, Jenerali Burhan aliapa kuung’oa utawala, na kuahidi kuheshimu haki za binadamu, kusitisha marufuku ya kutotoka nje, kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, kuvunjilia mbali Serikali zote za majimbo, kuwashtaki waliowaua waandamanaji na kukabiliana na rushwa.

Baraza hilo limewakamata baadhi ya waliokuwa maofisa wa Serikali na kuahidi kutowatawanya waandamanaji. Pia limeuomba upinzani kumchagua waziri mkuu mpya na kuahidi kumuidhinisha watakayemchagua. Wakati huo huo, Serikali ya Uganda imesema ipo tayari kumpatia hifadhi Bashir endapo ataomba kuishi humo baada ya kupinduliwa na jeshi.

Waziri wa Mambo Nje wa Uganda, Henry Okello Oryem ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kuwa endapo Uganda itaombwa kumpatia hifadhi, suala hilo litashughulikiwa katika kiwango cha juu cha uongozi wa nchi hiyo. Oryem alisema Uganda inatambua na kuheshimu kazi kubwa aliyoifanya Bashir katika kuleta amani na kupatikana kwa uhuru wa Sudan Kusini.

“Uganda haitaomba radhi wala kujutia hatua yake ya kuwa tayari kumuhifadhi Bashir,” alisema waziri huyo. Bashir anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kukiuka haki za kibinadamu na uhalifu wa kivita kwenye mgogoro jimboni Darfur.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles