28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Ole Gunnar Solskjaer Antivirus kwa Paul Pogba

BADI MCHOMOLO

OLE Gunnar Solskjaer ni kocha ambaye amebeba matumaini makubwa ya klabu ya Manchester United, baada ya kufukuzwa kazi kwa kocha Jose Mourinho, tangu Desemba 18, mwaka jana.

Kocha huyo alifukuzwa kazi kutokana na mwenendo mbaya wa timu.

Alifukuzwa kazi baada ya kuisimamia timu hiyo kwa jumla ya michezo 17 huku akishinda michezo saba ya Ligi Kuu na kuiacha ikiwa na pointi 19, hivyo nafasi yake ikachukuliwa na Ole Gunnar Solskjaer, mchezaji wa zamani wa kocha Sir Alex Ferguson.

Mbali na kupewa mkataba mfupi wa miezi sita kuifundisha timu hiyo kama kocha wa muda, lakini amebeba matumaini makubwa ya klabu pamoja na wachezaji ambao walikuwa na wakati mgumu chini ya Mourinho.

Miongoni mwa wachezaji hao ni Paul Pogba, ambaye alimtaja kuwa ni Kirusi ndani ya klabu na ndio maana timu ilikuwa inashindwa kufanya vizuri katika baadhi ya michezo yake hasa kwenye michuano ya Ligi Kuu.

Mourinho aliamua kuweka wazi kuwa, Pogba ni Kirusi, hivyo alimfanya akae nje ya uwanja katika baadhi ya michezo huku akidai kuwa hana msaada ndani ya kikosi na anacheza mpira wa kitoto.

Katika michezo 14 aliyocheza chini ya Mourinho msimu huu, mchezaji huyo aliweza kufunga mabao matatu kwenye ligi, hakuweza kumpa uhuru uwanjani japokuwa alikuwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Ufaransa na kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Urusi.

Pogba hakuwa na amani kabisa kuwa chini ya Mourinho tangu mgogoro wao ulipoanza mapema Februari mwaka jana, lakini baada ya ujio wa kocha mpya wa muda Solskjaer, kunamfanya Pogba aonekane mchezaji mpya mwenye uwezo wa hali ya juu.

Pogba sasa ana furaha na maisha yake ya soka, furaha hiyo inaweza kumfanya kusitisha mipango yake ya kuondoka ndani ya Manchester United, huku awali akihusishwa kutaka kujiunga na Barcelona, Real Madrid au klabu yake ya zamani ya Juventus.

Solskjaer anaonekana kuwa Antivirus kwa Pogba ambaye alionekana kuwa Virus kwa Jose Mourinho. Pogba katika michezo minne aliyocheza ya Ligi Kuu chini ya kocha huyo mpya, ameweza kufunga mabao manne, wakati chini ya Mourinho aliweza kufunga mabao matatu katika michezo 14.

Hata hivyo Solskjaer amemfanya mchezaji huyo kuingia kwenye historia ilioachwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo Wayne Rooney ya kufunga mabao mawili katika kila mchezo kati ya michezo miwili mfululizo ambapo Rooney alifanya hivyo Desemba 2012.

Kwa upande mwingine Pogba katika michezo hiyo miwili aliyoonyesha kipaji cha hali ya juu chini ya Solskjaer, aliweza kumfanya kocha wa zamani wa timu hiyo Ferguson kuinuka kwenye jukwaa na kumpigia makofi huku akionekana kuwa na uso wa furaha.

Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kocha huyo kuonekana akiwa na furaha ya aina hiyo mbele ya mashabiki tangu alipopata nafuu baada ya kusumbuliwa na tatizo la ubongo.

Ferguson alikuwa anasumbuliwa na tatizo hilo baada ya mishipa ya damu kupasuka kichwani na damu kuanza kuenea kwenye ubongo, hivyo kocha huyo alifanyiwa upasuaji Mei mwaka jana na sasa anaendelea vizuri na ana nguvu ya kwenda kuiangalia timu yake Man United pamoja na mchezaji wake wa zamani Solskjaer aliyopewa jukumu la kuwa kocha wa muda hadi mwishoni mwa msimu huu.

Solskjaer amemfanya Pogba kuwa na amani, amempa uhuru wa kufanya atakalo uwanjani hasa katika kuhakikisha anaisaidia timu, tayari ameonesha kuwa anaweza kuisaidia timu hiyo kwa kuwa aliambiwa acheze huku akiwa anaonesha anaupenda mpira, hivyo atafanya vizuri.

Kutokana na muda mchache tangu kuteuliwa kwa Solskjaer kuwa kocha mkuu, ameonekana kuwa Antivirus kwa Pogba ambaye alitajwa kuwa Virus katika maendelea ya timu, sasa mchezaji huyo anashirikiana vizuri na wachezaji wenzake kwa ajili ya kuipigania timu.

Kikubwa kinachoangaliwa ni nini atakifanya kocha huyo na wachezaji wake katika mchezo wa Ligi Kuu ujao Jumapili dhidi ya wapinzani wao Tottenham.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles