22.7 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Ofisi za TRA Kimara zaungua moto

1429769289-tra-logoNa KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), jana ililazimika kuhamishia ofisi zake Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam, baada ya ofisi zake zilizokuwa Kimara Baruti kuungua moto.

Tukio hilo lilitokea jana asubuhi na kusababisha huduma zilizokuwa zikitolewa kusimama kwa muda kabla ya kuhamishiwa Kimara Mwisho.

MTANZANIA lilifika eneo la tukio na kukuta wafanyakazi wa mamlaka hiyo, wakijaribu kuokoa nyaraka mbalimbali huku wananchi wakisaidia kuzima moto huo.

Kwa mujibu wa mashuhuda walioshuhudia tukio hilo, moto ulianza kuwaka saa 12 asubuhi katika baa ya jirani na ofisi hizo inayojulikana kwa jina la Hawaii.

Gabriel Mwaibuji ambaye ni mkazi wa maeneo ya Kimara Baruti, alisema walilazimika kuchota maji kwa kutumia ndoo ili kuhakikisha wanaziokoa ofisi hizo ambazo zilishaanza kuungua moto katika ukuta wa nyuma unaopakana na ofisi za TRA.

“Hatujui chanzo cha moto ila tulichosikia ni kelele kutoka kwa mmoja wa wafanya usafi katika baa hiyo ambaye alisema moto ulikuwa ukiwaka kwenye stoo tangu saa 12 lakini watu wa zimamoto wamekuja saa mbili na robo na kukuta tumeshafanya jitihada za kuupunguza kwani ulikuwa mkali sana kwa sababu paa lake limeezekwa kwa makuti ya mnazi,” alisema Mwaibuji.

Saturine Shao ambaye ni mmiliki wa baa ya Hawaii, alisema pamoja na baa pia alikuwa akiuza bia za jumla na vinywaji baridi ambavyo kwa ujumla wake thamani yake inaweza kufikia zaidi ya milioni 100.

Alisema hadi sasa hajui chanzo cha moto huo na kwamba anachohisi ni shoti ya umeme kutokana na taarifa alizopewa na mfanyakazi wake aliyekuwa akifanya usafi.

“Sina uhakika wa chanzo cha moto ila nahisi ni shoti ya umeme kutokana na kuwa msichana aliyekuwa akifanya usafi ndiye aliyenipigia na kuniambia kuwa moto unawaka stoo na kutokana na vitu vilivyokuwemo thamani yake inaweza kuwa zaidi ya milioni 100,” alisema Shao.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kinondoni, Wallace Mkande, alisema hakuna hasara iliyopatikana na badala yake watasitisha huduma hadi Jumatatu kutokana na kuwa wameamua kuzihamishia ofisi hizo maeneo ya Kimara Mwisho.

“Hasara tuliyopata ni kukosa kodi ambazo ilikuwa tukusanye leo (jana) na kesho lakini kuhusu vifaa kuungua tumefanikiwa kuvitoa na kwamba tutaendelea kuwahudumia wananchi kuanzia Jumatatu,” alisema Mnkande.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles