Ofisi ya Waziri Mkuu watakiwa kujituma

0
569

Mwandishi Wetu -Dodoma

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko, amekutana na watumishi wa ofisi hiyo kwa nyakati tofauti huku akiwataka kufanya kazi kwa ufanisi.

Akizungumza na watumishi hao jana Dodoma, aliwataka kuzingatia taratibu, sheria na kanuni za utumishi wa umma katika kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali.

Mwaluko alisema kuwa katika kuhakiksha utekelezaji unakuwa wa ufanisi, ataandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa hao ili kuboresha utendaji kazi wao.

“Maofisa ndio watu wanaoanza kuchakata shughuli nyingi za utekelezaji, taarifa za uratibu wa shughuli za Serikali zikiandaliwa vizuri kabla ya kumfikia mkurugenzi matokeo yake huwa ni mazuri.

“Niwasihi jitumeni na ongezeni umakini katika kutekeleza majukumu, pia shirikishaneni ili muweze kufanikiwa kutekeleza vyema jukumu la msingi la ofisi hii,” alisema Mwaluko.

Alisistiza ushirikiano katika utendaji wa majukumu usizingatie kada tu, au maofisa ndani ya idara na vitengo, bali ushirikiano pia uwe kati ya idara na vitengo, lengo ni kuhakikisha kila ofisa anakuwa na uwezo wa kumudu kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali kwa ufanisi.

Majukumu ya msingi yanayosimamiwa kwa sasa na ofisi hiyo ni uratibu wa shughuli za Serikali, kuongoza shughuli za Serikali bungeni, kuratibu maadhimisho na sherehe za kitaifa, usimamizi na uratibu wa shughuli za dharura na maafa.

Aidha ofisi hiyo ndiyo inaratibu shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi na maendeleo ya sekta binafsi, shughuli za kuwezesha maendeleo ya uwekezaji na shughuli za kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Shughuli nyingine zinazoratibiwa na kusimamiwa na ofisi hiyo ni mapambano dhidi ya janga la Ukimwi na usimamizi wa athari zake kwa Tanzania Bara, mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya, shughuli za uchaguzi nchini na masuala ya vyama vya siasa pamoja na uchapaji wa nyaraka rasmi za Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here