-DAR ES SALAAM
OFISI ya Makamu wa Rais, imekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameomba kujiuzulu nafasi yake jambo ambalo imesema ni uongo na uzushi mkubwa.
Taarifa za kiongozi huyo wa ngazi ya juu kutaka kujiuzulu zimetolewa na mwanaharakati, Mange Kimambi na baadae kusambazwa katika mitandao mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Makamu wa Rais, ilieleza kuwa uchochezi huo ulilenga kuliweka Taifa kwenye taharuki.
Kutokana na hali hiyo ilielezwa kuwa Makamu wa Rais yuko bega kwa bega na Rais, Dk. John Magufuli katika kufanya kazi zao kwa mujibu wa Katiba ili kuwaletea wananchi maendeleo.
“Ofisi ya Makamu wa Rais inawataka wananchi na Watanzania kwa ujumla kupuuza taarifa hiyo ambayo inalenga kupotosha umma kuhusu ushirikiano mzuri uliopo baina ya viongozi wetu.
“Mwisho Ofisi ya Makamu wa Rais inawasihi Watanzania kufanya kazi kwa bidii na wajiepushe na vitendo vinavyolenga kuvuruga amani na utulivu nchini,” alisema.
Katika taarifa iliyosambazwa na Mange, alidai kuwa amepata taarifa za ndani kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameomba kujiuzulu wadhifa wake kutokana na kile alichodai kugombezwa na mkuu wa nchi jambo ambalo lilizua maswali kutoka katika pembe mbalimbali nchini.